Sep 21, 2021 02:41 UTC
  • Rais Macron awaomba radhi Waislamu wa Algeria kwa jinai zilizofanywa na nchi yake nchini humo

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron jana Jumatatu aliwaomba radhi Waislamu wa Algeria kutokana na jinai ilizofanywa na Ufaransa katika nchi hiyo.

Rais Macron jana alikutana na Waislamu wa Algeria waliopigana vita vya ukombozi wa Algeria na kusema, katika siku za karibuni Ufaransa inatazamia kupasisha sheria ya kuwafidia wahanga wa jinai zilizofanywa na nchi yake huko Algeria.

Miezi kadhaa iliyopita Emmanuel Macron alitangaza kuwa hataomba radhi kuhusu jinai zilizofanywa na Ufaransa huko Algeria wakati nchi hiyo ilipoivamia Algeria na kwamba katu hataomba radhi kutokana na uvamizi uliofanywa na jeshi la Ufaransa huko Algeria katika karne ya ishirini. 

Japokuwa Algeria imekuwa ikiitaka Ufaransa iombe radhi kwa jinai ilizotenda dhidi ya binadamu wakati ilipoikoloni nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, lakini Paris ilikuwa imekataa kuomba radhi. 

Ufaransa iliikoloni Algeria kwa kipindi cha miaka 132.

Vita vya ukombozi wa Algeria viliendelea kuanzia mwaka 1954 hadi 1962 na watu zaidi ya milioni moja na nusu waliuliwa katika vita hivyo huku wapigania uhuru wa nchi hiyo wakikandamizwa na kunyanyaswa na majeshi ya Ufaransa. 

Ufaransa  pia ilifanya majaribio ya nyuklia nchini Algeria kuanzia mwaka 1960 hadi 1966; na kwa mujibu wa shirika la habari la Algeria majaribio hayo yalisababisha vifo vya Waalgeria 42,000 na kuwadhuru maelfu ya wengine sambamba na kuharibu mazingira nchini humo.

Tarehe 13 Februari 1960 Ufaransa ilifanya jaribio kubwa la bomu la nyuklia katika eneo la Reggane kusini mwa Algeria. Bomu hilo la nyuklia lilikuwa na nguvu mara tano zaidi ya bomu lililotumiwa na Marekani kufanya mashambulizi huko Hiroshima huko Japan. 

Jaribio la bomu la nyuklia la Ufaransa huko Reggane Algeria mwaka 1960 

 

Tags