Sep 21, 2021 07:00 UTC
  • Wamarekani wengi: Upo uwezekano wa kutokea vita vingine vya ndani Marekani

Karibu nusu ya Wamarekani wanaitakidi kuwa, upo uwezekano wa kutokea vita vingine vya ndani nchini humo.

William Gill na Darrell M. West wameeleza katika makala iliyochapishwa na Taasisi ya Brookings kwamba, kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa kote nchini Marekani mwaka huu wa 2021 na mkusanyamaoni John Zogby, idadi kubwa ya Wamarekani wanaokaribia asilimia 46 wanaamini kuwa, upo uwezekano wa kutokea tena vita vya ndani nchini humo.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, asilimia 43 ya waliotoa maoni yao wanaitakidi kuwa ni baidi kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani, wakati asilimia 11 ya Wamarekani wamesema hawana uhakika juu ya jambo hilo.

Makala hiyo iliyochapishwa tarehe 16 Septemba imejadili maudhui kadhaa za changamoto zinazoweza kusababisha Marekani kutumbukia kwenye lindi la vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Maudhui hizo ni pamoja na usawa wa kimbari baina ya watu wa rangi tofauti, udhibiti wa silaha moto, utoaji mimba, uhalali wa chaguzi zinazofanyika nchini humo, mabadiliko ya tabianchi, upigaji chanjo, uvaaji barakoa na masuala mengine ya kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa yanayozusha hasira na uadui baina ya Wamarekani wenyewe.

Gill na West wameendelea kueleza katika makala yao hiyo kwamba, mojawapo ya ishara za hali ya mvutano inayotia wasiwasi mkubwa zaidi ndani ya jamii ya sasa ya Marekani ni imani kubwa iliyopo kwamba upande wa pili, yaani serikali ni onevu na haina huruma.

Katika makala hiyo ya Taasisi ya Brookings imebainishwa kwamba, vita vya ndani nchini Marekani vilivyodumu kwa miaka minne katika muongo wa 1860, ambavyo vilikuwa ni hatua ya lazima kwa ajili ya kuondokana na utumwa, na ambavyo viliteketeza roho za watu zaidi ya laki sita, vilikuwa na athari angamizi kwa uchumi, mfumo wa kisiasa na jamii nzima ya Marekani na kwamba haipasi kufikiria kuwa tukio kama hilo halitatokea tena.../

Tags