Sep 21, 2021 07:40 UTC
  • Mawaziri wa EU waiunga mkono Ufaransa dhidi ya Marekani katika mzozo wa nyambizi

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrell amesema nchi wanachama wa umoja huo zimeonyesha uungaji mkono wao na mshikamano kwa Ufaransa katika mzozo wa nyambizi kati yake na Marekani.

Borrell amewaambia waandishi wa habari kuwa, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya, waliokutana mjini New York kando ya Mkutano Mkuu wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa, wameelezea wazi mshikamano wao na Ufaransa na uungaji mkono ulio dhahir.

Mgogoro unaohusiana na kuvunjika makubaliano ya Australia kununua nyambizi za nyuklia za Ufaransa kwa yuro bilioni 66 unaendelea kutokota. Ufaransa inailaumu Australia kuvunja mkataba huo kwa makusudi na kuanzisha ushirikiano mpya wa usalama na Marekani na Uingereza.

Joseph Borrell

Jumatano, tarehe 15 Septemba, maafisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon walisaini makubaliano na wenzao wa Uingereza ya kuipatia Australia nyambizi ya nyuklia, hatua ambayo imezikasirisha nchi nyingi duniani ikiwemo Ufaransa.

Katika kulalamikia makubaliano hayo, ambayo yamesababisha kufutwa mkataba uliosainiwa kati ya Ufaransa na Australia, ambapo Ufaransa ingeiuzia Australia nyambizi zenye thamani ya dola bilioni 66, Paris imechukua hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa, ya kuwaita nyumbani mabalozi wake wa Washington na Canberra.../

Tags