Sep 22, 2021 02:29 UTC
  • Rais wa Ufaransa awaomba radhi wananchi wa Algeria

Hatimaye baada ya kupita miongo mingi tangu Wafaransa watende jinai nchini Algeria na katika hali ambayo, kumekuwa kukifichuliwa nyaraka mpya za jinai hizo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amewaomba radhi wananchi wa Algeria na kuahidi kupasishwa sheria katika siku za usoni ambayo itatoa fidia kwa nchi hiyo ya Kiafrika.

Baada ya kupita zaidi ya miongo sita tangu kumalizika vita vya miaka minane baina ya jeshi vamizi la Ufaransa na wanapambano wa Algeria, katika miaka ya hivi karibuni kumefichuliwa nyaraka mpya zinazoonyesha jinai za Wafaransa huko Algeria, nyaraka ambazo zimezidi kuweka wazi na bayana dhulma na ukatili wa Wafaransa kwa wanamapambano wa Kialgeria.

Kwa mujibu wa nyaraka mpya kabisa zilizotolewa miezi michache iliyopita, zaidi ya Waalgeria milioni 1.5 waliuawa katika zama za ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria na katika vita vya kupigania uhuru katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Pamoja na hayo, majaribio ya nyuklia ya Ufaransa katika jangwa la Algeria pamoja na athari zake haribifu zilizobakia lilikuwa jambo hatari zaidi.

Moja ya jinai hizo za kutisha ni majaribio 17 ya nyuklia yaliyofanywa na Ufaransa katika jangwa la Algeria baina ya mwaka 1960 hadi 1966. Moja ya mifano ya jinai hizo ni hatua ya Wafaransa ya kuwafanya Walgeria 150 kuwa panya wa maabara baada ya kuwatundika katika nguzo kwenye eneo la majaribio ya nyuklia kwa ajili ya kufahamu ni kwa kiasi gani miale ya nyuklia ina taathira kwa mwili wa mwanadamu.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

 

Muhammad al-Raqqani, mmoja wa mashuhuda wa matukio hayo ambaye amefichua hayo katika miaka ya hivi karibuni anasema kuwa, wakati wa kufanyika majaribio ya nyuklia ya Ufaransa, kulitokea mlipuko ambao ulipelekea kuibuka wingu la moshi mfano wa uyoga baada ya mlipuko huo ambao ulielekea juu mbinguni huku kukitokea upepo mkali wenye kasi kubwa ambao ulielekea katika makazi ya watu ambapo hatukuwa na uwezo wa kuona umbali wa mita tatu.

Licha ya kufichuliwa jinai hizi, hakuna wakati ambao viongozi wa Ufaransa wamewahi kujitokeza na kuomba radhi rasmi. Hata ofisi ya Rais nchini Ufaransa hivi karibuni ilitangaza kuwa, Emmanuel Macron katu hataomba msamaha kutokana na Ufaransa kuikalia kwa mabavu Algeria. Msimamo huo wa Paris uliwakasirisha mno wananchi wa Algeria ambao wamesisitiza mara kadhaa kwamba, Ufaransa inapaswa kuomba radhi rasmi kutokana na jinai zake dhidi ya wananchi wa Algeria na pia kulipa fidia.

Hata hivyo ieleweke kwamba, jinai za Ufaransa barani Afrika hazikuishia tu kwa wananchi wa Algeria, bali akthari ya kaumu, mbari na mataifa ya Kiafrika yalikuwa wahanga wa jinai hizi. Ufaransa kama ilivyokuwa kwa madola mengine ya Ulaya, katika kipindi cha ukoloni yalikiuka waziwazi haki za binadamu barani Afrika kama ambavyo yalifanya pia mauaji ya kimbari. Vitendo hivi visivyo vya kibinadamu vingali vinaendelea hadi sasa.

Taswira za baadhi ya matukio ya mkoloni Mfaransa nchini Algeria

 

Nyaraka za kuaminika zinaonyesha kuwa, Ufaransa ilikuwa na mkono katika mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyotokea mwaka 1994 yanayotajwa kama moja ya mauaji makubwa zaidi ya kimbari katika karne ya 20. Mauaji hayo yaligharimu roho za watu 800,000 kutoka kabila la Watutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani. Kuna nyaraka nyingi pia zilizotolewa ambazo zinabainisha ukoloni wa Ufaransa katika mataifa kama Senegal, Ivory Coast na Benin. Mataifa hayo yaligeuzwa na Wafaransa na kuwa vituo vya biashara ya watumwa na katika kipindi cha mkoloni Mfaransa, vyanzo vya utajiri na maliasili za nchi hizo ziliporwa na wakoloni huo.

Filihali, wanasiasa wa Ufaransa wanafanya juhudi ambapo kwa kuomba msamaha wanataka kufutwa historia chafu ya mkoloni Mfaransa huko barani Afrika na hivyo kuimarisha nafasi ya nchi hiyo barani humo. Hata hivyo, kuomba msamaha huku kama hakutaambatana na kufidia makosa ya huko nyuma, bila shaka hakutakuwa na taathira hata chembe katika fikra za waliowengi.

Tags