Sep 22, 2021 10:25 UTC
  • Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Kikao cha 76 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilifungliwa jana tarehe 21 Septemba mjini New York huko Marekani kwa hotuba ya Katibu Mkuu wa umoja huo, Antonio Guterres.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi alihutubia kikao hicho jana kupitia njia ya video akieleza misimamo ya Iran kuhusu masuala muhimu ya kikanda na changamoto za kimataifa. Sehemu kubwa ya hotuba ya Rais Ebrahim Raisi katika hotuba yake kwenye siku ya kwanza ya kikao cha Baraza Kuu la UN ilichunguza sababu za migogoro inayotokea eneo la Magharibi mwa Asia na ulimwenguni kwa ujumla.

Tunapotupia jicho matukio ya miongo kadhaa ya karibuni katika eneo la Magharibi mwa Asia tunaona kuwa, siasa za Marekani ndio chanzo na sababu ya vita, uharibifu na machafuko mengi yaliyotokea katika eneo hilo hususan huko Afghanistan, Iraq na Yemen. Sera na siasa hizo za Marekani zimepekea kuuawa maelfu ya watu wasio na hatia wakiwemo wanawake na watoto wadogo, kuwalazimisha mamilioni kuwa wakimbizi, kuharibu miundombinu ya uchumi na uzalishalishaji, kuneza umaskini, ukosefu wa amani na ugaidi na matatizo mengine mengi. Vilevile jeraha la miaka mingi la Palestina na kukaliwa kwa mabavu ardhi hiyo tukufu bado ni kadhia muhimu ya Umma wa Kiislamu, na jeraha hilo limetoneshwa zaidi kwa usaliti wa baadhi ya nchi za Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel.

Akifafanua baadhi ya ukweli huo mchungu, Rais Ebrahim Raisi amesema, Israel ndiyo taasisi kubwa zaidi ya ugaidi wa kiserikali ambayo inatoa maagizo ya kuuawa wanawake na watoto wa Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi huko Palestina, na hii leo imelifanya eneo la Gaza kuwa jela kubwa zaidi duniani kutokana na kulizingira eneo hilo kutoka pande zote za angani, habarini na nchi kavu. 

Baraza Kuu la UN

Sera za uharibifu za Marekani haziishii katika kuuhami na kuusaidia kwa hali na mali utawala wa Israel unaoua watoto na wanawake. 

Marekani hususan katika kipindi cha utawala wa Donald Trump ilianzisha vita kubwa ya kiuchumi dhidi ya taifa la Iran kwa shabaha ya kuliwekea mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi. Sera hizo haribifu zinaendelezwa katika kipindi cha utawala wa Joe Biden ambaye pia jana alihutubia kikao cha 76 cha Baraza Kuu na kudai kuwa nchi yake iko tayari kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Wakati wa mapambano ya dunia dhidi ya maambukizi ya kirusi cha corona pia Iran imeendelea kulengwa kwa vikwazo vya kidhalimu vya Marekani na kuzuiwa kupata vifaa na hata chanjo ya kukabiliana na kirusi hicho. Hata hivyo hii leo Iran inahesabiwa kuwa mmoja kati ya wazalishaji wa chanjo ya corona duniani licha ya vikwazo vya Marekani na nchi za Ulaya.

Katika masuala ya kikanda pia Iran imefanikiwa kupanua zaidi uhusiano wake wa kigeni hususan na nchi jirani licha ya njama za Marekani za kutaka kuitenga Jamhuri ya Kiislamu. Katika mkondo huo, kukubaliwa uanachama wa Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kunahesabisa kuwa tukio muhimu linaloonesha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina nafasi kubwa na muhimu katika siasa za kikanda na taathira kubwa katika kuimarisha amani na usalama wa kieneo.

Katika sehemu moja ya hotuba yake kwenye kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema, kuondoka bila ya mpangilio Marekani katika nchi ya Afghanistan kumezitia gharama nchi za kanda hiyo na kuogeza kuwa, nafasi ya Iran katika kanda ya Magharibi mwa Asia hususan katika nchi za Iraq na Syria imefanikisha kuangamiza ugaidi katika eneo hilo kwa msaada wa makamanda Abu Mahdi al Muhandis na Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, hotuba ya jana ya Rais Ebrahim Raisi kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imejikita zaidi kwenye masuala mawili muhimu:

Mosi ni kwamba, chanzo cha matatizo na migogoro mingi ya ulimwengu kama umaskini, ukosefu wa amani, vita na machafuko ya kisiasa ni tamaa ya madola ya kibeberu na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja. Suluhisho la tatizo hili ni kubadilishwa sera hizo katika upeo wa kimataifa na kuelewa vyema vitisho na changamoto zilizopo sambamba na kuwa na sera shirikishi na maamuzi jumuishi chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Suala la pili katika hotuba ya Rais Ebrahim Raisi ni sisitizo lake la udharura wa kuwajibika katika kushughulikia vitisho na changamoto za kimataifa. Rais wa Sayyid Ebrahim Rais amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutoa mchango wake katika juhudi za kujenga dunia bora zaidi yenye utawala wa busara na mantiki, uadilifu, maadili ya kibinadamu na inayojali masuala ya kiroho.