Sep 22, 2021 12:37 UTC
  • Taliban yaomba ipewe nafasi ya kuhutubia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Serikali ya muda ya Taliban imeuandikia barua Umoja wa Mataifa kuomba ipewe nafasi ya kuhutubia mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la umoja huo unaoendelea hivi sasa makao makuu ya UN mjini New York.

Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema, Katibu Mkuu Antonio Guterres alipokea barua ya Taliban siku ya Jumatatu ya ombi la kutaka ipewe nafasi ya kushiriki katika mazungumzo ya ngazi ya juu ya taasisi hiyo.

Shirika la habari la Reuters, limethibitisha kuona nakala ya barua hiyo, ambayo ndani yake, Taliban imemtambulisha Suhail Shaheen msemaji wake katika ofisi ya kisiasa iliyoko mjini Doha, Qatar kuwa ndiye balozi mpya wa Afghanistan katika Umoja wa Mataifa.

Suhail Shaheen

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa, ombi la Taliban la kutaka ipatiwe kiti cha uwakilishi wa Afghanistan na kuhutubia Baraza Kuu la umoja huo litajadiliwa katika kamisheni maalumu ya UN inayoundwa na nchi tisa wanachama.

Tangu Taliban iliposhika hatamu za madaraka nchini Afghanistan mnamo arehe 15 Agosti hakuna nchi yoyote hadi sasa iliyoiitambua serikali iliyoundwa na kundi hilo.../