Sep 23, 2021 04:37 UTC
  • Baada ya kuongezeka mzozo, wakuu wa majeshi ya Marekani na Russia wakutana Finland

Baada ya kupamba moto mzozo katika uhusiano wa Marekani na Russia na kuingia kwenye hatua hatari na kufikia hadi viongozi wa Washington kusema kuwa Russia ni adui mkubwa wa Marekani kuliko China, juhudi za kupunguza mivutano hiyo zimeanza kuchukuliwa kupitia kukutanishwa wakuu wa majeshi ya nchi hizo mbili katika mji mkuu wa Finland, Halsinki.

Shirika la habari la Associated Press limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Jenerali Valery Gerasimov mkuu wa majeshi ya Russia na Jenerali Mark Milley, mkuu wa majeshi ya Marekani wamekutana mjini Halsinki, Finland na kujadiliana masuala mbalimbali yakiwemo ya Afghanistan, hasa baada ya kundi la Taliban kuidhibiti nchi hiyo.

Ripoti hiyo imesema kuwa, mazungumzo ya wakuu hao wa majeshi ya Russia na Marekani yamefanyika katika hali ambayo Russia inaishutumu Marekani kwa kufanya njama za kujiimarisha kijeshi katika nchi zinazopakana na Afghanistan na za karibu na Russia.

Rais Vladimir Putin wa Russia (kushoto) na mwenzake wa Marekani, Joe Biden

 

Uhusiano wa Marekani na Russia umeharibika sana katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kutokana na masuala mbalimbali ikiwemo kujipenyeza kijeshi Marekani katika maeneo ambayo yalikuwa ni uwanja wa ushawishi mkubwa wa Russia kama vile Ukraine.

Marekani imeiwekea Russia vikwazo vya upande mmoja kwa madai tofauti yakiwemo ya Ukraine na kisiwa cha Crimean kilichojitenga na Ukraine na kujiunga na Russia.

Serikali ya Moscow nayo imekuwa ikichukua hatua na misimamo ya kulipiza kisasi kwa kila hatua inayochukuliwa na Marekani na waitifaki wake wa Magharibi hasa nchi za Ulaya ambazo nazo zinatumia madai mbalimbali kuiweka chini ya mashinikizo Russia.

Tags