Sep 23, 2021 10:46 UTC
  • Mawaziri wa G4 wataka Baraza la Usalama la UN lifanyiwe marekebisho

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa G4, kundi linaloundwa na nchi za India, Brazil, Ujerumani na Japan wametaka kufanyiwa mabadiliko ya kimsingi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mwito huo wameutoa leo Alkhamisi pembeni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakitaka kuongezwa idadi ya wanachama wa kudumu na wasio wa kudumu wa baraza hilo. Mawaziri hao wamesema, mabadiliko hayo yatauwezesha Umoja wa Mataifa kukabiliana vizuri na changamoto tata zinazotokea na kuusaidia kulinda usalama na amani kimataifa kwa ufanisi zaidi.

Taarifa ya pamoja ya mawaziri wa kundi hilo imesema, suala la kufanyiwa marekebisho Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kipaumbele cha haraka hivi sasa kwani baraza hilo haliendani na uhalisia wa mambo ulivyo duniani leo. Wamesema nchi zilizoendelea na zinazoendelea kwa kasi zimeongezeka hivi sasa na nchi hizo ni wanachama muhimu wa Umoja wa Mataifa hivyo kuna udharura wa kufanyiwa mabadiliko ya haraka na ya kimsingi, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Felix Tchisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 

 

Wakati huo huo, jana, Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambaye ni mwenyekiti wa hivi sasa wa Umoja wa Afrika AU aliwasilisha malalamiko kadhaa ya bara hilo katika mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ulioanza juzi mjini New York, likiwemo suala la bara la Afrika kupatiwa uanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la umoja huo.

Tshisekedi ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi za Afrika kuhutubia mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, alizungumzia masuala yanayolihusu bara la Afrika na kuthibitisha mahitaji ya uwakilishi bora wa bara hilo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Tags