Sep 23, 2021 10:53 UTC
  • Wasiopiga chanjo wazidi kuambukizwa corona nchini Uingereza

Duru za habari zimeripoti kuwa, watu wengi wanaoambukizwa zaidi ugonjwa wa corona au UVIKO-19 nchini Uingereza hivi sasa ni wale wanaokataa kupiga chanjo.

Shirika la habari la IRIB limewanukuu wataalamu wa magonjwa ya kuambukiza wakisema kuwa, jamii ya vijana wa Uingereza ambao hawajapiga chanjo za corona ndio wanaoambukizwa zaidi ugonjwa huo. Wengine wanaokumbwa na ugonjwa huo katika nchi hiyo ya Ulaya ni wale wanaopinga kuwepo ugonjwa wa UVIKO-19 na wasiochunga miongozo inayotolewa na watu wa afya. Hiyo imetajwa kuwa ndiyo sababu ya kuongezeka maambukizo ya corona nchini Uingereza hivi sasa.

Idadi iliyotolewa na serikali ya wagonjwa wa UVIKO-19 nchini Uingereza hadi hivi sasa ni zaidi ya milioni 7 na laki 5 na 30,103. Uingereza ni ya nne duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na UVIKO-19 baada ya Marekani, India na Brazil. Aidha Uingereza ni ya kwanza katika bara zima la Ulaya kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo na wagonjwa wa corona. Idadi ya watu waliopoteza maisha kwa UVIKO-19 nchini Uingereza hadi leo mchana kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali ya London walikuwa ni 135,621.

Chanjo ya UVIKO-19 ni moja ya njia bora za kujikinga na ugonjwa hatari wa corona

 

Aidha kwa kuzingatia idadi ya watu wake, Uingereza inahesabiwa kuwa moja ya nchi zilizopoteza watu wengi zaidi na kuathiriwa vibaya zaidi na UVIKO-19 duniani.

Kwa upande wa dunia, idadi ya watu waliokuwa wameshaambukizwa corona hadi leo mchana duniani walikuwa ni  230,950,876. Kati ya hao, 4,734,397 walikuwa wameshafariki dunia na 207,650,810 walikuwa wameshapona.

Tags