Sep 24, 2021 02:16 UTC
  • Juhudi za Biden za kujaribu kupunguza mvutano baina ya Marekani na Ufaransa

Kufuatia mazungumzo ya simu ya Marais Joe Biden wa Marekani na Emmanuel Macron wa Ufaransa hapo siku ya Jumatano, viongozi hao wametoa taarifa ya pamoja wakisema wameamua kuendelea na mashauriano kwa ajili ya kutatua hitilifu zilizojitokeza baina ya pande mbili kuhusu mkataba wa kiusalama wa AUKUS.

Hii ni pamoja na kuwa Rais Macron wa Ufaransa amekubali kumrejesha balozi wa nchi hiyo mjini Washington. Uamuzi huo umefikiwa baada ya Biden kukiri kwamba kama mashauriano yangefanyika na Ufaransa kabla ya kutangazwa rasmi mkataba huo wa usalama na Australia yangeweza kuepusha mvutano wa kidiplomasia uliopo hivi sasa na Paris. Pamoja na hayo nchi mbili zimekubaliana kuendeleza mashauriano kwa ajili ya kukarabati na kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Kufuatia mvutano wa karibuni kati ya Paris na Washington juu ya kufutiliwa mbali mkataba wa Australia kununua nyambizi 12 za nyuklia kutoka Ufaransa na hatimaye kuamua kununua nyambizi nane za aina hiyo kutoka Marekani, viongozi wa Ufaransa wamekosoa na kulaani vikali jambo hilo. Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ameyataja mapatano hayo ya Washington na Canberra kuwa usaliti mkubwa. Kwa mtazamo wa Wafaransa, kwa hatua yake hiyo, Biden amethibitisha wazi kwamba angali anafuata siasa zilezile zilizoanzishwa na mtangulizi wake Donald Trump za kuitanguiliza Marekani katika kila jambo yaani, 'Marekani Kwanza.'

Mkataba wa AUKUS unafuatilia kuzidhibiti China na Russia

Kufuatia hatua hiyo Paris imewaita nyumbani mabalozi wake kutoka Washington na Canberra na wakati huohuo kufutilia mbali vikao vyote vilivyokuwa vimepangwa awali kufanyika kati yake na viongozi wa Marekani na Uingereza. Msimamo huo wa Ufaransa umeungwa mkono na Umoja wa Ulaya. Brussels imesema mapatano ya pande tatu za Marekani Uingreza na Australia na vilevile kufutiliwa mbali mkataba wa silaha na Ufaransa ni jambo lisilokubalika.

Kwa mtazamo wa Umoja wa Ulaya, serikali ya Biden ilipuuza mikataba mikongwe ya Ulaya katika mapatano ya kiusalama ya AUKUS, na kuamua kushirikiana tu na nchi zinazozungumza Kiingereza kwa ajili ya kukabiliana na China. Katika kulalamikia suala hilo, Brussels imeamua kufuata stratijia mpya katika eneo la Indo-Pacific ambayo kwa hakika inaashiria kuchukuliwa maamuzi huru kuhusu eneo hilo la kistratijia.

Elise Labott, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, raia wa Marekani anasema: Biden anafuatilia urithi wa siasa za nje alizoachiwa na Trump, mfano wa wazi ukiwa ni usaliti wa karibuni wa Marekani dhidi ya Ufaransa kuhusu mkataba na Australia, ambapo alikanyaga moja kwa moja maslahi ya mshirika wake mkongwe na hivyo kudhuru pakubwa uaminifu wa washirika wake wengine.

Radiamali hiyo hasi ya Ulaya dhidi ya Marekani hatimaye imeipelekea Washington kuiliwaza Paris ambapo viongozi wa serikali ya Biden wamekuwa wakitoa matamshi ya kuonyesha jinsi Ufaransa ilivyo na umuhimu mkubwa kwa Marekani. Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema Ufaransa ni mshirika mkubwa wa Marekani katika eneo la Indo-Pacific. Mbali na hayo Biden amefanya juhudi kubwa za kuzungumza na Emannuel Macron wa Ufaransa ambapo mazungumzo ya simu ya Jumatano ilikuwa aina fulani ya Marekani kuiomba msamaha Ufaransa.

Nyambizi ya kijeshi

Pamoja na hayo, hatua ya karibuni ya serikali ya Biden kutoishirikisha Ulaya na hasa Ufaransa katika mkataba wa kiusalama wa AUKUS ni suala linaloonyesha kuwa Marekani bado haijabadilisha msimamo wake kuhusu nchi za Ulaya. Hata Uingereza ambayo ilikuwa na mataumaini makubwa ya kuwa na uhusiano maalumu na Marekani baada ya Brexit, sasa imejipata katika hali ngumu ambapo haijapewa nafasi yoyote ya maana katika sera za nje za Marekani wala katika uhusiano wa pande mbili na kwa hivyo imeachwa ikisubiri tu na kuendelea kuwa na matumaini ya Washington kutekeleza ahadi zake na kutazamwa kwa jicho la huruma na Wamarekani.

Hii ndio maana nchi muhimu za Ulaya na hasa Ujerumani zimefikia uamuzi kwamba zinapasa kufuata sera huru katika nyanja za usalama, siasa za nje na kujidhaminia nishati.

Tags