Sep 24, 2021 07:43 UTC
  • Programu ya ujasusi ya Israel imedukua simu za mawaziri wasiopungua 5 wa Ufaransa

Imefichuliwa kuwa programu ya ujasusi ya Israel ya Pegasus imedukua na kufanya ujasusi katika simu za rununu (mobile phone) za mawaziri wasiopungua 5 wa serikali ya Ufaransa.

Uchunguzi uliofanywa na huduma za kiufundi za Ufaransa umebaini kuwepo alama zinazotia shaka katika simu za kinganjani za mawaziri kadhaa wa nchi hiyo wakiwemo mawaziri wa elimu, kilimo, ustawi na nyumba. 

Ni baada ya gazeti la Le Monde kutangaza hivi karibuni kuwa simu ya kinganjani ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa imedukuliwa na kufanyiwa ujasusi kwa kutumia programu ya kijasusi ya Israel, Pegasus. 

Uchunguzi uliofanywa na mashirika 17 ya habari yanayofanya kazi chini ya kundi lisilo la kiserikali la Forbidden Stories lenye makao makuu yake mjini Paris na ambalo lilichapisha matokeo ya uchunguzi huo mwezi Julai mwaka huu unaonyesha kuwa programu hiyo iliyotengenezwa kwa kibali cha shirika la utawala haramu wa Israel la NSO, imefanikiwa au kufeli kudukua simu erevu za waandishi, maafisa wa serikali na wanaharakati wa haki za binadamu wapatao 37 na kwa ujumla imeweza kutumika kulenga simu zisizopungua elfu 50 katika maeneo tofauti duniani.

Wanasiasa mashuhuri kimataifa kama Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Charles Michel, Rais wa sasa wa Baraza la Ulaya ni miongoni mwa wahanga wa programu hiyo ya ujasusi ya Israel.

Macron, mmoja kati ya wahanga wa ujasusi wa Pegasus

Kwa mujibu wa ripoti ya CNBC, miongoni mwa watu waliolengwa kwa kutumia programu hiyo ya kijasusi ya Israel ni aliyekuwa mchumba wa Jamal Khashoggi, mwandishi na mkosoaji wa utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia aliyeuawa mwaka 2018 kwa njia ya kutisha kwa amri ya moja kwa moja ya mrithi wa ufalme wa nchi hiyo, Muhamamd bin Salman.   

Tags