Sep 25, 2021 07:20 UTC
  • Taliban yasisitiza nia yake ya kustawisha uhusiano na Iran na Russia

Msemaji wa kundi la Taliban ametaka kustawishwa uhusiano wa pande mbili kati ya kundi hilo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia.

Zabihullah Mujahid amesisitiza kuwa, serikali ya muda ya kundi la Taliban nchini Afghanistan haina hitilafu yoyote na Tehran na inataka kuwa na uhusiano imara na Iran.

Mujahid, ambaye pia na naibu waziri wa habari na utamaduni wa serikali ya muda ya Taliban amezungumzia pia uhusiano wa kundi hilo na Russia na akasema, serikali ya kundi hilo inataka kuwa na uhusiano wa kiwango cha juu pia na Russia.

Aidha amesema, Russia inaweza kuwa na nafasi ya upatanishi kati ya Umoja wa Mataifa na Afghanistan katika kupunguza mashinikizo ya vikwazo dhidi ya kundi la Taliban.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov (katika) na viongozi wa Taliban

Msemaji wa Taliban amegusia pia suala la genge la kigaidi la DAESH (ISIS) na akasema, kuwepo Daesh nchini Afghanistan si lolote si chochote na kwamba wapiganaji wa Taliban hivi sasa wanaendelea kuchukua hatua za kusaka na kutambua maficho ya genge hilo.

Zabihullah Mujahid amesisitiza pia kuwa, Marekani imeahidi kwamba haitafanya shambulio jengine lolote dhidi ya ardhi ya Afghanistan katika siku za usoni.

Tarehe 15 Agosti, kundi la Taliban lilishika hatamau za madaraka nchini Afghanistan; na Marekani, baada ya miaka 20 ya kuwepo kijeshi nchini humo, iliondoka rasmi katika ardhi ya Afghanistan ikiwa imedhalilika na kufedheheka.../

Tags