Sep 25, 2021 11:01 UTC
  • Udharura wa kuchunguzwa jinai zilizofanywa na Marekani na Uingereza nchini Afghanistan

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imetoa ripoti ikithibitisha kuwa majeshi vamizi ya Marekani, shirika la NATO na Uingereza yenyewe yameua raia nchini Afghanistan.

Ripoti hiyo imesema kuwa, watoto 86 na zaidi ya raia wengine 200 wa Afghanistan wameuawa katika mashambulizi ya wanajeshi vamizi huko Aghanistan. Japokuwa Wizara ya Ulinzi ya Uingereza haijaweka wazi ripoti hiyo ilitolewa lini, lakini ripoti nyingine za vyombo vya kujitegemea zilizotolewa katika kipindi cha miongo miwili ya uvamizi wa Marekani na washirika wake huko Afghanistan zimetoa takwimu zenye idadi kubwa zaidi ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo waliouawa na majeshi ya nchi hizo za Magharibi.

Kulenga raia kimakosa badala ya wapiganaji wa Taliban ikiwa ni pamoja na kushambulia sherehe za harusi au mikusanyiko ya wananchi kama shambulizi lililofanywa na majeshi ya Ujerumani dhidi ya mkusanyiko wa raia waliokuwa wakiteka maji huko Kunduz, sambamba na kutumia silaha zilizopigwa marufuku ni miongoni mwa vielelezo vya mauaji mengi yaliyofanywa na majeshi hayo vamizi dhidi ya raia wa Afghanistan. Vilevile maelfu ya raia wa nchi hiyo wamejeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu. 

Profesa Mark Hirald wa Chuo Kikuu cha New Hampshire huko Marekani amezungumzia jinai za kutisha zilizofanywa na nchi yake huko Afghanistan na kueleza kuwa, kuna udharura wa kufunguliwa faili la wahanga wa mashambulizi ya majeshi ya Marekani huko Afghanistan, kwa sababu idadi ya raia waliouawa katika mashambulizi hayo ni kubwa sana na ya kutisha. Kwa kadiri kwamba, mwanajeshi Robert Bells wa jeshi hilo amekiri kwamba, yeye peke yake aliua raia 16 wa Afghanistan katika vijiji viwili vya Kandahar huko kusini mwa Afghanistan na kwamba wengi wao walikuwa wanawake na watoto.

Rais wengi wa kawaida wameuawa bila ya hatia yoyote. 

Katika kipindi cha utawala wa Hamid Karzai na Muhammad Ashraf Ghani kuliundwa kamati ya kutafuta ukweli kuhusu mauaji yaliyofanywa na wanajeshi wa Marekani na washirika wake nchini Afghanisgtan ambayo baada ya kuthibitisha kufanyika jinai hiyo, nchi hizo za Magharibi zilitosheka tu kwa kutoa vijihela vya kutuliza mambo na kuomba radhi kwa njia ya kudhalilisha bila ya kuundwa tume ya kimataifa ya kuchunguza na kushughulikia suala hilo. 

Kukata vidole vya mikono na viungo tofauti vya raia wa Afghanistan ilikuwa miongoni mwa tafrija na burudani za wanajeshi vamizi wa Marekani na Uingereza, jambo ambalo baada ya kufichuliwa na vyombo huru na vya kujitegemea vya habari, limezusha wimbi kubwa la hasira na malalamiko baina ya Waafghani.

Sayyid Jawad Hussein ambaye ni miongoni mwa wanasiasa watajika wa Afghanistan amelaani jinai na uhalifu mkubwa uliofanywa na wanajeshi vamizi nchini humo katika kipindi cha miongo miwili iliyopita na ametoa wito wa kufuatiliwa kadhia hiyo katika mahakama za kimataifa. Sayyid Jawad anasema: Wamarekani wameua kwa umati familia nyingi za Waafghani kwa kisingizio kwamba ni Mataliban au Daesh na mauaji hayo yanapaswa kushughulikiwa. 

Maelfu ya wanavijiji wa Afghanistan wameuwa katika mashambulizi ya Marekani na NATO

Alaa kulli hal, tunaweza kusema kuwa, kutolewa ripoti ya Wizara ya Ulinzi ya Uingereza kuhusu mauaji ya raia wa Afghanistan ni aina fulani ya kutaka kupunguza ukubwa wa jinai zilizofanyika nchini humo na ili kuzuia kutolewa ripoti pana na kamili zaidi ya vyombo huru na vya kujitegemea au asasi za kimataifa kuhusu uhalifu uliofanywa na majeshi ya nchi za Magharibi nchini Afghanistan.

Kwa msingi huo watu wa Afghanistan wanatarajia kuwa, taasisi huru na jumuiya za kimataifa zitafanya uchunguzi kamili wa kudhihirisha sura halisi ya jinai na uhalifu uliofanywa na Marekani, Uingereza na washirika wao nchini Afghanistan na kutayaisha mazingira ya kufikishwa wahalifu hao katika mahakama za kimataifa.  

Tags