Sep 26, 2021 04:33 UTC
  • Uchaguzi muhimu wa Jumapili ya leo na mustakbali wa Ujerumani

Leo Jumapili Wajerumani wanashiriki katika uchaguzi muhimu wenye ushindani mkali ambao ni nadra sana kuonekana katika chaguzi ziizofanyika nchini humo.

Uchunguzi wa maoni unaonesha kuwa, mgombea wa chama cha Social Democrats (SPD) atashinda kinyang'anyiro hicho. Hata hivyo tofauti ndogo sana iliyopo baina ya wagombea wa kiti cha Kansela wa Ujerumani yumkini ikapelekea kubadilika matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo. 

Uchaguzi wa leo ni miongoni mwa chaguzi muhimu sana nchini Ujerumani katika miongo ya karibuni. Uchaguzi huu wa sasa unaonekana kuwa na umuhimu wa kihistoria tangu baada ya kuungana Ujerumani mbili mwanzoni mwa muongo wa 1990 kutokana na kuwa, Angela Merkel anang'atuka madarakani baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 16 huku Ujerumani ikisumbuliwa na migogoro mtawalia. Vyama vitatu vya siasa vimearifisha wagombea wa kiti cha Kansela wa Ujerumani katika uchaguzi wa leo. Wagombea Armin Laschet kutoka chama cha Christian Democratic Union ambaye pia ni Waziri Mkuu wa jimbo lenye idadi kubwa ya watu la North Rhine-Westphalia, Olaf Scholz kutoka chama cha Social Democrats (SPD) ambaye ni Waziri wa Fedha na Naibu Kansela, na Annalena Barbock kutoka Chama cha Kijani wamekuwa wakichuana katika kampeni za uchaguzi kwa miezi kadhaa sasa kwa ajili ya kunasa kiti cha Kansela wa Ujerumani. 

Katika uchaguzi wa sasa hakuna mgombea mwenye ushawishi mkubwa sana kama ule wa Angela Merkel aliyeiongoza Ujerumani kwa awamu na vipindi vinne mfululizo na kubakia katika nafasi hiyo muda mrefu zaidi kuliko mwanasiasa yoyote mwingine wa Ujerumani. Kwa msingi huo, inaonekana kuwa Wajerumani watapigia kura mipango na sera za wagombea. Miongozi mwa sera zilizotangazwa na wagombea hao watatu katika kampeni za uchaguzi ni pamoja na umuhimu wa kutiliwa maanani mabadiliko ya tabianchi na kupunguza gesi za sumu, ustawi wa elimu na kutoa huduma za serikali na za kijamii kupitia mtandao wa intaneti.

Suala la suhuru pia ni miongoni mwa mambo yaliyopewa mazingatio katika kampeni za wagombea wa vyama hivyo vitatu. Chama cha Christian Democratic Union kimeahidi kupunguza shinikizo la ushuru kwa raia wa tabaka la kati na wenye kipato cha chini na kuzidisha ushuru kwa vipato vya juu; ilhali chama cha Social Democrats (SPD) kimetoa pendekezo la kuzidisha asilimia moja ya ushuru wa wenye vipato vikubwa na kupambana na ukwepaji wa ushuru. Sera za Chama cha Kijani katika uchaguzi wa leo zinashabihiana na zile za chama cha SPD.

Kuwepo kwa wahjiri nchini Ujerumani ni miongoni mwa mijadala iliyotawala kampeni za uchaguzi wa leo. Suala hilo limemulikwa sana kutokana na ukweli kuwa, hatima ya wahajiri na kiwango cha kukubalika kwao katika jamii ya Ujerumani vina umuhimu mkubwa sana kwa mustakbali wa uchumi wa nchi hiyo.

Christian Lindner ambaye ni kiongozi wa chama cha Free Democratic Party (FDP) anasema kuhusu kadhia hii kwamba: Ujerumani inahitajia wahajiri wachapakazi na hodari na tunapaswa kuchagua wahajiri hao kwa mujibu wa mahitaji yetu ya kiuchumi.

Vyama vitatu vinavyochuana katika uchaguzi wa leo huko Ujerumani vina mitazamo tofauti kuhusiana na jinsi ya kushughulikia suala la wahajiri.

Suala la wahajiri limezusha mjadala mkubwa katika kampeni za uchaguzi

Katika suala la siasa za nje, chama cha Social Democrats kinasisitiza udharura wa kuundwa jeshi moja la Ulaya na kuimarishwa nafasi ya mawaziri wa mambo ya nje katika kuchukua maamuzi. Kwa upande wake Chama cha Kijani kimetetea suala la kujihusisha zaidi Ujerumani katika masuala ya kimataifa na kusisitiza kuwa, Berlin inapaswa kuwa nguvu yenye harakati kubwa wakari wa migogoro ya kisiasa lakini si kwa kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na ya kitaifa.

Kwa vyovyote vile, Jumapili ya leo ni siku muhimu sana kwa Ujerumani na Umoja wa Ulaya kwa ujumla. Maambukizi ya virusi vya corona, kudhoofika uchumi wa nchi nyingi za Ulaya, mustakbali wa uhusiano wa Ulaya na Marekani, migogoro kama ile ya wimbi la wakimbizi na wahajiri na kadhalika vinazidisha mzigo wa Kansela ajaye wa Ujerumani.

Kwa kutilia maanani hali hiyo inaonekana kuwa, mrithi wa nafasi ya Angela Merkel anakabiliwa na kibarua kigumu.  

Tags