Sep 26, 2021 08:01 UTC
  • Guterres: Sasa ni wakati wa kutokomeza silaha za maangamizi za nyuklia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, sasa ni wakati wa kuondoa silaha za nyuklia kutoka kwenye ulimwengu huu, na kuanzisha zama mpya za mazungumzo, uaminifu na amani.

António Guterres amesema hayo leo, katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya kukomesha silaha za nyuklia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa kushughulikia tishio la silaha za nyuklia “imekuwa msingi wa kazi ya umoja huuo tangu kuanzishwa kwake, lilipopitishwa azimio la kwanza la Baraza Kuu kuhusu silaha hizo mwaka 1946 likitaka "kuondolewa silaha zote za atomiki na silaha zingine zote  zinazoweza kusababisha maangamizi makuu kote duniani."

António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

 

Hata hivyo, Antonio Guterres amesema, ingawa idadi ya silaha za nyuklia zimekuwa zikipungua kwa miongo kadhaa, zingine 14,000 zimehifadhiwa kote ulimwenguni, na kuifanya dunia kukabiliwa na hatari kubwa zaidi ya nyuklia kwa karibu miongo minne. "Nchi zinaendelea kuimarisha vituo vya silaha za nyuklia, na tunaona ishara zenye kutia wasiwasi za mashindano mapya ya silaha. Ubinadamu bado unaendelea kuwa karibu na silaha za maangamizi ya nyuklia suala ambalo halikubaliki”, ameeleza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Alkhamisi hivi majuzi Katimu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alitoa wito pia kwa nchi zote zinazomiliki teknolojia ya nyuklia kutia saini mkataba wa kina wa kupiga marufuku matumizi ya nyuklia (CTBT), ambao ulipitishwa mwaka 1996, na umesainiwa na nchi 185