Sep 28, 2021 03:11 UTC
  • Al Kadhimi: Arubaini ya Imam Hussein ni kilele cha upinzani dhidi ya ukiukaji wa haki za binadamu

Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa shughuli ya siku ya Arubaini ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) ni kilele cha upinzani wa wanadamu dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mustafa al Kadhimi ambaye jana alishiriki katika kumbukumbuku ya siku ya Arubaini tangu baada ya kuuliwa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali (as) katika mkoa wa Karbala amesisitiza kuwa shughuli hiyo inayowashirikisha mamilioni ya watu ndiyo malalamiko makubwa zaidi ya binadamu dhidi ya ukiukaji na ukandamizaji wa haki za binadamu.

Amesema kuwa, Arubaini ya Imam Hussein na masahaba zake wema ndiyo mjumuiko mkubwa zaidi wa binadamu wa kuonyesha upinzani endelevu dhidi ya haki za binadamu katika historia. 

Waziri Mkuu wa Iraq amesema Arubaini ya Imam Hussein ni sisitizo kwamba, kukabiliana na ukandamizaji na ukiukaji wa haki za binadamu si jambo rahisi.

Wakuu wa mkoa wa Karbala nchini Iraq walisema mapema jana kuwa, takwimu za awali zinaonesha kwamba wafanyaziara ya Arubaini ya Imam Hussein AS mwaka huu katika Haram ya mtukufu huyo ni zaidi ya watu milioni 14.

Shirika la habari la FARS limewanukuu wakuu wa mkoa huo wakisema kwamba idadi ya wafanyaziara ya Arubaini ya Imam Hussein mwaka huu wa 1443 Hijria imepindukia watu milioni 14. 

Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein bin Ali (as).

Mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) aliuawa shahidi mwaka 61 Hijria katika ardhi ya Karbala nchini Iraq akiwa pamoja na familia na masahaba zake 72 wakipambana dhidi ya dhulma na upotoshaji uliokuwa ukifanywa na mtawala wa wakati huo, Yazid bin Muawiya katika mafundisho ya dini ya Uislamu.

Historia inasema mtu wa kwanza kuzuru kaburi la mtukufu huyo alikuwa Sahaba wa Mtume Muhammad (saw) Jabir bin Abdillah al Ansari ambaye alifika Karbala na kuzuru kaburi la Imam Hussein katika siku ya arubaini tangu baada ya mauaji yake. 

Tags