Sep 30, 2021 02:23 UTC
  • Mgogoro wa nishati Uingereza, nembo ya kushindwa serikali ya Wahafidhina

Mgogoro wa mafuta na uhaba wa petroli nchini Uingereza ni mkubwa kisasi kwamba magari yamekuwa yakihujumu vituo vya mafuta kwa ajili ya kupata bidhaa hiyo muhimu lakini bila mafanikio, jambo ambalo hatimaye limeipelekea serikali ya Wahafidhina kulitaka jeshi liwe tayari kuingilia kati ili kuokoa hali ya mambo.

Ili kukabiliana na hali hiyo, jeshi limewekwa tayari kwa ajili ya kukabiliana na mgogoro wowote wa kijamii unaoweza kuzuka kufuatia hali hiyo na pia madereva wa malori ya jeshi tokea Jumanne wamekuwa wakipewa mafunzo maalumu ya kusaidia kujaza mafuta vituo vya petroli ili kukidhi mahitaji ya magari ya raia.

Kama ilivyotarajiwa baada ya kuondoka Uingereza katika Umoja wa Ulaya, Brixit, nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na migogoro tofauti. Kufuatia Brixit, uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya Brussels na London umeharibika sana. Kwa kutilia maanani kwamba Umoja wa Ulaya ni mshirika mkuu wa Uingereza katika masuala ya biashara na hudumu za msingi, ilitabiriwa tangu mwanzo kuwa kujiondoa Uingereza katika umoja huo kungeisababishia nchi hiyo matatizo mengi. Kuhusiana na suala hilo na kwa miezi kadhaa sasa, Uingereza inakabiliwa na matatizo mengi ya kudhaminia raia wake bidhaa na huduma za msingi.

Foleni ndefu za magari kwenye vituo vya mafuta nchini Uingereza

Mbali na kukosekana bidhaa muhimu katika maduka ya jumla katika baadhi ya miji ya Uingereza, sasa kuadimika bidhaa ya petroni katika vituo vingi vya mafuta na kuonekana foleni ndefu za magari katika vituo hivyo ni mambo yanayoendelea kutoa mashinikizo dhidi ya serikali ya London. Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza amejaribu kupunguza mashinikizo hayo kwa kudai kuwa matatizo hayo hayatokani na Brixit bali yanatokana na tatizo la kuenea nchini vurusi vya corona na tatizo la Covid-19. Pamoja na hayo lakini ni wazi kuwa matatizo ya hivi sasa ya Uingereza yanatokana na Brixit na kuwa tatizo la corona ni kichocheo tu ambacho kimezidisha matatizo hayo.

Matatizo hayo yameibua tatizo jingine nalo ni la uhaba wa madereva wa malori makubwa ambao umekuwa na taathira hasi katika mfumo wa kudhamini bidhaa za msingi kama vyakula, nishati na bidhaa nyinginezo muhimu. Inatabiriwa kuwa kama tatizo hilo halitatatuliwa katika siku kumi zijazo basi mwenendo wa kusambaza bidhaa za chakula nchini pia utakabiliwa na matatizo makubwa.

Kuongezeka vikwazo vya serikali ya London dhidi ya wasomi na wataalamu wahajiri kutoka nchi za kigeni na hasa kutoka Ulaya Mashariki, kumepunguza idadi ya wafanyakaza wa kazi za mikono na za sulubu na wale walio na ujuzi mdogo wakiwemo madereva wa malori  ya uchukuzi wa bidhaa. Kwa hakika moja ya taathira za moja kwa moja za Brixit ni kupungua idadi ya wafanyazi wahajiri nchini Uingereza. Chama cha madera wa malori ya uchukuzi na usafirishaji wa bidhaa nchini Uingereza kimesema kuwa kwa sasa kuna upungufu wa madera laki moja wanaopasa kuhudumu katika sekta hiyo.

Brian Madderson, mkuu wa chama cha wauza mafuta ya petroli Uingereza anasema: Inaonekana tatizo hili la uhaba wa petroli litaendelea kwa muda mrefu.

Msongamano wa magari kwenye vituo vya mafuta kufuatia uhaba wa bidhaa hiyo muhimu Uingereza

Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, serikali ya London itatoa vibali vya muda kwa madereva zaidi ya 5000 kutoka nje ili waje wasaidie katika utatuzi wa tatizo la uhaba wa madereva nchini, jambo ambalo limekuwa likifuatiliwa kwa muda mrefu na wahusika wa sekta hiyo lakini serikali ikawa inalipinga.

Kwa mtazamo wa Umoja wa Ulaya na wataalamu wengi wa bara hilo, kujiondoa Uingereza katika umoja huo kulitabiriwa kuandamana na matatizo ya hivi sasa yanayoikabili nchi hiyo. Kwa hakika kinyume na walivyoahidiwa Waingereza wakati wa kujitoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya kwamba wangenufaika na mambo mengi ya kuboresha maisha yao, sasa serikali ya Wahafidhina hata imeshindwa kuwadhaminia bidhaa za msingi kabisa maishani na inatapatapa isijue la kufanya katika uwanja huo. Hii ni katika hali ambayo uchumi wa Uingereza pia umedorora na wala hakuna dalili yoyote inayoonyesha kuwa utaimarika karibuni. Jambo hilo bila shaka litakuwa na taathira hasi za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa serikali ya London.

Tags