Oct 06, 2021 03:05 UTC
  • Dmitry Polyansky
    Dmitry Polyansky

Naibu mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali (OPCW) linaelekea kuwa wenzo wa kisiasa unaotumiwa na nchi za Magharibi kwa ajili ya kuzinyanyasa nchi nyingine.

Dmitry Polyansky amekiambia kikao cha Baraza la Usalama la UN kwamba, nchi za Magharibi zinalitumia shirika hilo kama wenzo wa kisiasa wa kulipiza kisasi dhidi ya Syria na kuwanyanyasa viongozi wa nchi hiyo. 

Mwanadiplomasia huyo wa Russia ameongeza kuwa, sera za viongozi wa sekretarieti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kemikali (OPCW) kuhusu faili la Syria zimetupilia mbali msingi wa kutopendelea upande wowote na ni wazi kuwa zinaamiliana na baadhi ya masuala kwa matashi ya kisiasa.

Dmitry Polyansky amekumbusha kuwa, kutokana na misimamo kama hiyo OPCW inaelekea kuwa kuwa fimbo ya kisiasa katika mikono ya nchi za Magharibi inayotumiwa kuzinyanyasa nchi nyingine wapinzani wa Magharibi.

Amesema msimamo kama huu haukubaliki kwa taasisi ya kimataifa na kwamba faili la Syria halipasi kufungamanishwa tena na masuala ya silaha za kemikali.    

Tags