Oct 08, 2021 00:39 UTC
  • Biden akiri kuhusu kubaki nyuma uchumi wa Marekani; dalili ya kuporomoka nchi hiyo

Akizungumza karibuni katika jimbo la Michigan, Rais Joe Biden wa Marekani amesema nchi nyingine za dunia ziko mbioni kuishinda Marekani katika nyanja nyingi. Amesema licha ya kuwa Marekani bado inauongoza ulimwengu kiuchumi lakini inaendelea kupoteza taratibu nafasi yake hiyo.

Rais Biden amesema katika miaka 25 iliyopita, Marekani imekuwa katika nafasi ya kwanza kimataifa katika ustawi wa viwanda lakini hivi sasa haiko tena kwenye nafasi hiyo. Amesema maudhu hiyo inatoa ujumbe maalumu kwa washindani wake ambao wanafanya juhudi kubwa za kutaka kuishinda Marekani kiuchumi.

Kukiri rais wa Marekani kwamba nchi yake inafanya vibaya kiuchumi ni jambo linalojadiliwa na weledi wa mambo katika mazingira ya kudhoofika na hatimaye kuporomoka Marekani. Hapa tunapasa kuzingatia viashiria tofauti vya kiuchumi na kijamii vinavyoainisha mambo nchini Marekani.

Biden amesema kwa muda mrefu Marekani imekuwa ikiongoza ulimwengu katika nyanja za miundombinu bora lakini kwa sasa nchi hiyo iko katika nafasi ya kumi na tatu kati ya nchi zilizo na miundomsingi bora na imara duniani. Vilevile amesema Marekani imekuwa katika mstari wa kwanza kati ya nchi zilizo na elimu bora ya vyuo vikuu lakini hivi sasa na kwa mujibu wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumim na Ustawi nchi hiyo inashikilia nafasi ya 35 kimataifa.

Rais Biden amepatwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kuporomoka uchumi wa Marelani

Suala la tatu ambalo Biden amelazimika kukiri kwamba linaonyesha kuwa Marekani imerudi nyuma kimaendeleo, ni suala la uzalishaji wa viwanda. Rais wa Marekani amelinganisha uzalishaji wa viwanda kati ya nchi yake na China na kukiri kuwa Marekani imewachwa nyuma katika uwanja huo.

Kwa mujibu wa Biden, katika miaka 20 iliyopota mashirika ya uzalishaji chuma nchini Marekani yamepungua kutoka mashirika 100 hadi 51 na nafasi za ajira katika sekta hiyo pia kupungua kwa asilimia 40 tokea mwaka 2000. Hii ni katika hali ambayo kwa sasa China inazalisha katika mwezi mmoja pekee kiwango cha chuma ambacho kinazalishwa na Marekani mwaka mzima. Biden vilevile ameashiria idadi kubwa ya magari yanayozalishwa na China ikilinganishwa na Marekani na kusema suala hilo linaloashiria wazi kuwa nchi hiyo ya Magharibi imaeachwa nyuma na China katika suala la ustawi wa viwanda.

Matamshi hayo ya rais wa Marekani yanathibitisha wazi kwamba mwenendo wa kudhoofika Marekani kiuchumi ni suala lisilofichika tena na kwamba mwenendo huo umepata kasi kubwa katika miaka ya karibuni na hasa baada ya kuenea duniani virusi vya corona. Mike Mullen, mkuu wa zamani wa kamandi ya majeshi ya Marekani anaahiria matatizo mengi yanayoikabili Marekani ukiwemo ubaguzi wa rangi, tofauti kubwa katika utoaji mishahara, dhulma inayofanyika katika ugavi wa pato la nchi na utovu wa maadili katika jamii na kusema: Sisi hatuendelei bali hebu niwe mkweli hapa; tunaendelea kudhoofika na kudidimia.

Hivi sasa China ambayo ni nguvu ya pili kubwa kiuchumi duniani, inafanya juhudi kubwa za kuipiku Marekani na kuwa katika nafasi ya kwanza kiuchumi ulimwenguni. Utabiri unaonyesha kuwa kufikia mwaka 2030 China itakuwa nguvu ya kwanza kiuchumi duniani. Kuthibiti jambo hilo na kushindwa Marekani kiuchumi bila shaka kutakuwa na matokeo hasi kwa nchi hiyo ambayo yataifanya kupoteza nafasi na itibari yake kisiasa na kiuchumi katika ngazi za kimataifa.

Vita vya kiuchumi kati ya Marekani na China

Hii ni mbali na kuwa dola ambayo ni sarafu yenye nguvu zaidi katika miamala ya kiuchumi duniani itapoteza nafasi hiyo na hivyo kuinyima Marekani fursa ya kuitumia kama chombo cha mashinikizo dhidi ya mataifa mengine. Marekani ambayo inatumia dola kama silaha ya vikwazo dhidi ya nchi nyingine, haitakuwa tena na uwezo wa kutoa mashinikizo ya vikwazo dhidi ya wapinzani na washindani wake.

Kwa msingi huo tunaweza kusema kwamba kuporomoka Marekani kiuchumi kunadhihiri katika sura tofauti ikiwemo ya kukabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti ya serikali kuu, kupungua kiwango cha mabadilishano ya kibiashara mkabala na nchi nyingine muhimu za kiuchumi na hasa China, kuongezeka deni la kitaifa hadi kufikia dola trilioni 28, kupungua nafasi ya dola katika mabadilishano ya fedha duniani, kupungua uzalishaji wa viwanda na kuongezeka mwenendo wa kuchakaa miundomsingi ya nchi hiyo ya kibeberu duniani.

Tags