Oct 09, 2021 07:56 UTC
  • Sergei Lavrov
    Sergei Lavrov

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia amesema kuwa nchi wanachama katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Maghribi (NATO) zinapaswa kubeba jukumu kuu la kuijenga upya Afghanistan.

Sergei Lavrov amekiambia kikao cha Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Ulaya kwamba nchi wanachama wa NATO ndizo zinazopaswa kubeba jukumu kuu la kuijenga upya nchi iliyoharibiwa na vita ya Afganistan na kuongeza kuwa, juhudi za Marekani na nchi nyingine wanachama wa NATO za kutaka kuzitwisha nchi nyingine mzigo wa wakimbizi wa Afghanistan si sahihi na hazikubaliki.

Itakumbukwa kuwa mwezi Agosti mwaka huu vikosi vya majeshi ya Marekani na waitifaki wake wa Magharibi vililazimika kuondoka Afghanistan baada ya kundi la Taliban kuudhibiti tena mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul. Marekani na wanachama wengine wa NATO waliivamia nchi hiyo na kuikalia kwa mabavu kwa miaka 20 wka kizingizio cha kupambana na ugaidi. 

Takwimu zinaonesha kuwa, uvamizi huo wa Marekani haukuwa na matunda yoyote ghairi ya kuzidisha machafuko, madawa ya kulevya, uharibifu wa miundombinu na mauaji ya maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan. Katika kipindi hicho wanajeshi 2,448 wa Marekani wameuawa wakiwa vitani, na vilevile wanajeshi 1144 wa shirika la NATO wameuawa katika vita hivyo.     

Tags