Oct 11, 2021 02:28 UTC
  • Ufaransa yakiri makosa yake ya kushiriki katika mashambulio ya Libya

Akizungumza karibuni katika mji wa Montpellier na viongozi wa nchi za Kiafrika za eneo la Sahel, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amekiri kwamba nchi yake ilifanya makosa kwa kushiriki katika mashambulio ya kijeshi yaliyofanyika dhidi ya Libya nwaka 2011.

Akizungumzia matukio ya eneo la Sahel barani Afrika na katika kujibu swali la vijana wa eneo hilo kuhusiana na nafasi ya Ufaransa katika kuvuruga usalama wa eneo hilo, Macron amesema: 'Sisi tuliivamia Mali mwaka 2013 si kwa ajili ya kulinda maslahi yetu tu ingawa ninaafikiana na nyinyi kuhusu suala la Libya. Ufaransa iliingilia masuala ya Libya bila kuzingatia mtazamo na maoni ya watu wa nchi hiyo. Uingiliaji huo hatimaye ulipelekea kuangushwa mfumo wa Muammar Gaddafi na sisi hatukuheshimu mamlaka ya nchi yoyote.'

Kukiri Macron kuhusu makosa yaliyofanywa na nchi hiyo kwa kushiriki kwake katika mashambulio yaliyofanyika dhidi ya Libya mwaka 2011, kwa hakika ni katika msururu wa matamshi yake kuhusu hatua za kikoloni na jinai zilizotekelezwa na Ufaransa barani Afrika na kuomba kwake msamaha kuhusu suala hilo.

Macron akiwa na baadhi ya viongozi wa Afrika

Mara tu baada ya kuanza harakati na mapambano ya watu wa Libya dhidi ya Mummar Gaddafi, dikteta wa nchi hiyo na kuanza mapigano kati ya wapinzani na jeshi lililokuwa likiimuunga mkono Gaddafi, Ufaransa ilishirikiana na nchi nyingine wanachama wa Nato, zikiwemo Marekani na Uingereza katika kuendesha mashambulio ya kijeshi ambayo hatimaye yaliangusha utawala wa Gaddafi na kupelekea kuuawa kwake na wapinzani. Pamoja na hayo lakini jambo hilo halikuleta mabadiliko yoyote yenye manufaa kwa watu wa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Kwa hakika tangu kung'olewa madarakani utawala wa dikteta Gaddafi, Libya inakabiliwa na ghasia na machafuko mengi ya umwagaji damu na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yasiyo na mwisho, ambapo hali hiyo imeyavutia makundi ya kigaidi yakiongozwa na Daesh kuifanya nchi hiyo kuwa kituo muhimu cha kuendeshea operesheni zao za kigaidi. Katika hatua ya baadaye serikali mbili hasimu na zinazoungwa mkono na nchi tofauti za kigeni ziliundwa katika miji tofauti ya nchi hiyo moja ikiwa ni ya umoja wa kitaifa yenye makao yake mjini Tripoli na nyingine inayoongozwa na jenerali mstaafu wa jeshi Halifa Haftar katika mji wa Benghazi na hivyo kuibua mapigano makali ya ndani ambayo hayajakuwa na faida yoyote kwa watu wa Libya isipokuwa hasara na maafa.

Ufaransa imekuwa ikiiunga mkono serikali ya Haftar mkabala wa serikali ya umoja wa kitaifa yenye makao makuu yake mjini Tripoli na ambayo inatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa kuwa serikali halali ya Libya. Michel Duclou, mchambuzi wa Ufaransa anasema: Katika miaka ya karibuni Ufaransa imekuwa ikituma askari maalumu kwenda kumsaidia kijeshi Haftar nchini Libya au hata kufanya nchini humo mashambulio ya ndege za kivita kwa maslahi yake.

Nafasi ya Ufaransa katika kuzikoloni nchi nyingi za bara la Afrika katika karne zilizopita na sasa kwa kutuma barani humo askari jeshi kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi hasa katika maeneo ya kaskazini na magharibi mwa bara hilo, daima imekuwa ni nafasi hasi. Katika miaka ya karibuni, Rais Macron amelazimika kukiri hadharani makosa yaliyofanywa na nchi yake barani Afrika. Kwa mfano mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, Macron alikiri kuhusika nchi yake katika mauaji ya halaiki yaliyotokea Rwanda mwaka 1994.

Mauaji ya kimbari Rwanda

Kukiri Macron kuwa Ufaransa ilishiriki katika mauaji ya kimbari ya Rwanda tena baada ya kupita miaka 27 tangu kufanyika maafa hayo makubwa ni dalili nyingine ya ukiukaji wa haki za binadamu na jinai kubwa zinazotekelezwa na nchi za Magharibi barani Afrika. Kabla ya hapo pia Macron alilazimika kukiri kuhusu mauaji ya umati na jinai kubwa zilizofanywa na Ufaransa huko Algeria lakini pamoja na hayo alikataa kuomba msamaha.

Kwa hakika faili la jinai za Ufaransa, ambayo ni miongoni mwa nchi za Magharibi zinazodai kuwa katika mstari wa mbele katika kutetea haki za binadamu, kuhusu vita vya kupigania uhuru wa Algeria ni jeusi kiasi kwamba haliwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile. Nukta ya kuzingatia hapa ni kuwa kungali kuna mvutano mkubwa kati ya Ufaransa na Algeria kuhusu suala hilo. Pamoja na hayo kukiri Macron kuhusu mauaji ya umati na makosa ya kijinai yaliyofanywa na nchi yake barani Afrika hakuwezi kuchukuliwa kuwa ni kubadilishwa sera za Ufaransa kuhusu bara la Agfrika bali nchi hiyo ya Magharibi inaendelea kufanya jinai nyingine za kutisha dhidi ya binadamu katika nchi tofauti za Afrika na Asia Magharibi.

Tags