Oct 12, 2021 02:33 UTC

Kiongozi mmoja mwandamizi wa Bunge la Russia amesema kuwa, ugomvi uliopo hivi sasa bina ya Marekani na China kuhusu Taiwan unaweza kuzusha mapigano ya kijeshi baina ya nchi hizo mbili na hata kupelekea kuzuka Vita vya Tatu vya Dunia.

Gazeti la kila siku la Izvestia linalochapishwa mjini Moscow, jana Jumatatu lilimnukuu Aleksey Pushkov, mmoja wa wajumbe wakuu wa Kamati ya Kisiasa na Kijasusi ya Baraza la Shirikisho yaani Baraza la Sanate la Russia akisema kuwa, anakubaliana na mtazamo kwamba, ugomvi uliopo hivi sasa baina ya Marekani na China kuhusu Taiwan, unaweza kuzusha Vita vya Tatu au vya Nne vya Dunia.

Kwa mara ya kwanza mtazamo huo ulitolewa juzi Jumapili na Dk Robert Farley, mwandishi wa Marekani ambaye alisema kwenye makala yake kwamba ugomvi uliopo hivi sasa baina Washington na Beijing kuhusiana na Taiwan ni wa hatari sana na unaweza kupelekea kutokea mapigano ya kijeshi baina ya nchi mbili.

Kuna hatari ugomvi wa Marekani na China ukaitumbukiza dunia katika Vita vya Tatu vya Dunia

 

 

Kwa mtazamo wa mwandishi huyo mkubwa na maarufu, kuna uwezekano Marekani na China zikaanzisha vita vya kugombania Taiwan na hata kama Marekani itashinda, basi viongozi wa China hawatoacha kamwe kampeni zao za kuhakikisha Taiwan inarejea kwenye ardhi ya China.

Seneta Aleksey Pushkov wa Russia ameifasiri makala hiyo na kuiwekwa kwenye ukurasa wake wa Telegram akisema kuwa, Marekani huwa haitumii akili wala busara, haina uvumilivu, huku China nayo haiko tayari kuachana na siasa zake za kupenda makuu na tayari imeshasubiri muda mrefu kufanikisha ndoto yake ya kuirejesha Taiwan kwenye ardhi ya China.

Muda wote huu Marekani imekuwa ikiingilia masuala ya Taiwan, kusaidia kifedha na kijeshi wafuasi wake na kuwachochea wafanye mambo yaliyo dhidi ya China.

Tags