Oct 12, 2021 12:02 UTC
  • Ungamo la Josep Borrell la kupungua ushawishi wa Umoja wa Ulaya

Hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuifuata kibubusa Marekani imeitilia alama ya swali utendaji na mamlaka ya uchukuaji maamuzi ya umoja huo katika medani za kimataifa.

Josep Borrel, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya ametahadharisha juu ya kubadilika asasi hiyo na kuwa mwanasesere wa kisiasa.

Borrel ameandika katika blogu yake kwamba: Hii leo, madola ya Ulaya yanakabiliwa na mwenendo hatari wa kugeuka na kuwa wenzo wa kisiasa badala ya kuwa mchezaji muhimu wa kisiasa katika uga wa kimataifa; Umoja wa Ulaya badala ya kuwa ni muundaji wa matukio, sasa umekuwa mtoa radiamali (majibu) tu kwa maamuzi ya watu wengine.

Katika hali ambayo, Josep Borrel anakiri Umoja wa Ulaya kutumiwa kama wenzo katika masuala mbalimbali ya kimataifa, katika miaka ya hivi karibuni, umoja huo umekuwa ukifuata matakwa ya Marekani moja baada ya jingine. Misimamo ya Umoja wa Ulaya mkabala na China, Russia na Iran ni ushahidi wa wazi jambo hili.

Katika hali ambayo, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kama walivyosema viongozi wa Ulaya ni moja ya mafanikio makubwa kabisa ya kisiasa ya Ulaya katika miaka ya hivi karibuni, umoja huo haujaweza kabisa kutekeleza ahadi ulizofunga nazo kwa mujibu wa makubaliano hayo. Umoja wa Ulaya umeonyesha kuwa, hauna uwezo wowote wa kimaamuzi mbele ya Marekani. Fauka ya hayo, Umoja wa Ulaya umeshindwa hata kutekeleza kivitendo ahadi zake katika fremu ya kuanzisha INSTEX yaani mfumo maalumu wa mabadilishano ya fedha kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Umoja wa Ulaya. Kwa maneno mengine ni kuwa,  masuala mawili ya JCPOA na INSTEX yameweka bayana ukweli huu kwamba, Umoja wa Ulaya ni kipando cha baadhi ya madola makubwa zaidi kiuchumi duniani, hivyo hauwezi kufanya biashara na Iran pasi na idhini na ruhusa ya  Marekani.

 

Udhaifu huu hauhusiani tu na kadhia ya mahusiano ya Umoja wa Ulaya na Iran, bali hata kuhusiana na China na Russia, umoja huo unafuata kikamilifu siasa za Marekani. Katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa Washington  wamefanya juhudi za kuufanya Umoja wa Ulaya nao uifuate Marekani katika siasa zake zilizo dhidi ya China. Juhudi za kuyafanya madola ya Ulaya yawe mguu kwa mguu na Marekani kwa ajili ya kukabiliana na hatua za China katika Ukanda wa Mashariki mwa Asia na himaya na uungaji mkono wa kijeshi wa Washington katika Bahari ya Kusini  ya China na langobahari la Taiwan na hatimaye kuwekewa vikwazo na Brussels baadhi ya viongozi wa Beijing ni moja ya mifano hiyo ya wazi ya viongozi wa Ulaya kufuata kibubusa sera za Ikulu ya White House.

Utendaji wa kindumakuwili na wa upande mmoja wa Marekani na Umoja wa Ulaya, umekwenda mbali zaidi kiasi kwamba, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, baada ya mvutano wa kijeshi wa Marekani na Australia amewahutubu viongozi wenzake wa Ulaya akisema: Marekani inafuatilia maslahi yake tu, hivyo madola ya Ulaya yanapaswa kupata funzo na hivyo kuchukua yenyewe jukumu la ulinzi. Indhari hizi kwa hakika ni ishara ya wazi ya wasiwasi mkubwa walionao viongozi wa Ulaya kuhusiana na Marekani kuyatumia mataiafa hayo kama wenzo wa kufikia malengo yake ya kisiasa dhidi ya China.

Kuhusiana na Russia pia, kufuata siasa za Marekani, kumeifanya hali ya mambo kuwa ni kwa madhara kwa Ulaya. Katika hali ambayo, ujirani unalazimu Umoja wa Ulaya kuwa na uhusiano mwema na wa amani na utulivu na Russia, miezi ya hivi karibuni imeshuhudia kushadidi uingiliaji wa Marekani katika masuala yanayohusiana na Russia,  na hivyo kuathiri maslahi ya Ulaya.

Bendeya ya Umoja wa Ulaya

 

Kwa mfano, ushindani wa kisiasa na kiusalama wa Marekani na Russia umepelekea Ulayai ukumbwe na kizingiti katika kunufaika na nishati ya Russia hususan vyanzo vikubwa vya nishati ya gesi ya Moscow. Hali hii, imeyafanya maisha ya mamilioni ya watu wa Ulaya ambao wanatemegea nishati rahisi na safi kukabiliwa na hatari.

Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana Charles Michel, Mkuu wa Baraza la Umoja wa Ulaya ameashiria matokeo mabaya ya  mizozo na hitilafu baina ya Washington na Moscow na kusema kuwa, Umoja wa Ulaya unapasa kuwa na mamlaka zaidi ya kuchukua maamuzi na uwezo wa kuchukua hatua katika uga wa kimataifa.

Pamoja na hayo, tajiriba na uzoefu unaonyesha kuwa,  madola ya Ulaya hayana azma na irada ya kutosha ya kuwa na siasa ambazo si tegemezi na zisizofungamana na Marekani au kwa uchache kupunguza hali yake ya utegemezi kwa Washington. Na katika mustakabli unaotabirika Umoja wa Ulaya kama alivyosema mkuu wake wa sera za kigeni ni kuwa, umoja huo utaendelea kuwa mwanasesere wa kisiasa wa watu wengine.

Tags