Oct 14, 2021 08:51 UTC
  • Ombi la Taliban kwa Russia kwa ajili ya kushiriki katika ujenzi mpya wa Afghanistan

Kundi la wanamgambo wa Taliban linaloongoza huko Afghanistan limetangaza kuwa linafanya mashauriano na Russia ili kupanua ushirikianao na kusaidiwa katika kuijenga upya nchi hiyo.

Dhabihullah Mujahid Msemaji wa kundi la Taliban amesisitiza katika mahojiano na shirika la habari la Tass kwamba kundi hilo linataraji kuwa Russia itashiriki katika kuijenga upya Afghanista ambayo imepata hasara na maafa makubwa katika miongo kadhaa iliyopita. Mujahid amesisitiza kuwa Taliban inataka kushirikiana na nchi zote na kwamba uwekezaji wa nchi za nje utakuwa na nafasi muhimu katika uwanja huo. 

Msemaji wa Taliban, Dhabihullah Mujahid 

Msemaji wa kundi la Taliban ameongeza kuwa, Russia ni nchi muhimu kwa upande wa kiuchumi. Afghanistan imeathirika vibaya wakati wa vita na Russia na nchi nyingine zinaweza kutoa mchango na kusaidia katika ujenzi mpya wa nchi hiyo. 

Matamshi ya Dhabihullah Mujahid Msemaji wa Taliban kuhusu ombi lao kwa Russia wakiitolea wito nchi hiyo iwe mshirika katika kuijenga upya Afghanistan yametolewa ikiwa ni katika muendelezo wa siasa za kundi hilo za kutaka kuwa na maelewano na kushirikiana na nchi hasimu za Marekani zikiwemo Russia na China katika kuijenga upya Afghanistan. 

Afghanistan katika miongo kadhaa iliyopita iliathiriwa na ukaliaji mabavu wa nchi ajinabi na vita vya ndani; na kwa sababu hiyo nchi hiyo inahitaji misaada kutoka nje na kushiriki nchi nyingine katika ujenzi mpya wa nchi hiyo kufutia kuharibiwa na kubomolewa pakubwa miundo mbinu ya nchi hiyo. Aidha kundi hilo ambalo liliingia madarakani tarehe 15 Agosti mwaka huu baada ya kuiangusha serikali ya Rais Ashraf-Ghani na kuudhibiti mji mkuu Kabul sasa linakabiliwa na kibarua kigumu cha kurekebisha uharibu mkubwa uliofanyika katika miundombinu  ya nchi hiyo; na kwa msingi huo linapasa kutoa kipaumbele na kuzingatia suala la kuijenga upya nchi hiyo ili kuboresha uchumi wake na kupiga hatua kuelekea ustawi na maendeleo ya nchi hiyo.  

Rais Ashraf-Ghani wa Afghanistan aliyeikimbia nchi baada ya Taliban kudhibiti Kabul 

Kwa msingi huo serikali ya Taliban ambayo inatambua vyema matatizo ya uhaba wa fedha uliopo na kupungua misaada ya kimataifa kwake inafanya kila iwezalo ili kuzishawishi nchi mbalimbali za eneo na kimataifa kushirikiana nayo katika ujenzi mpya wa Afghanistan; ambapo katika fremu ya siasa za kundi hilo China na Russia ambao ni mahasimu wa Marekani kimataifa ni kati ya machaguo ya awali ya kundi la Taliban katika uwanja huo.

Wakati huo huo Russia na China pia zina hamu ya kuwepo huko Afghanistan baada ya kujulikana ni kwa namna gani Taliban itatekeleza demokrasia na msingi wa jamhuri nchini humo na dhamira yake ya kuasisi serikali shirikishi nchini kwa kuzingatia kugonga mwamba sera za Marekani huko Afghanistan na kuondoka nchini humo kwa fedheha; na kwa njia hiyo ziweze kuwa na ushawishi katika duru mpya ya kisiasa katika nchi hiyo. 

Marekani ikiondoa wanajeshi wake Afghanistan 

Kushindwa Marekani kutimiza nara na ahadi zake kuhusu kupambana na ugaidi na pia kurejesha demokrasia nchini Afghanistan kumeipelekea jamii ya nchi hiyo kuwa na sababu nzuri ya kukubali uwepo na ushiriki wa nchi wapinzani wa Marekani zikiwemo China na Russia. Aidha Russia ambayo inafahamu vyema kuwa wananchi wa Afghanistan hawana dhana nzuri na Warussia kutokana na Umoja wa Kisovieti kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa kipindi cha muongo mmoja inajaribu kuandaa fursa ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi mpya wa Afghanistan na kusaidia kudhamini mahitaji ya watu wa nchi hiyo; na hivyo taratibu iweze kubadili dhana hiyo hasi ya wananchi wa Afghanistan kwa kujenga uhusiano mpya baina yake na serikali mpya ya Afghanistan chini ya uongozi wa Taliban. 

Katika mazingira hayo, inaonekana kuwa Taliban inaweza kupata msaada wa kuijenga upya Afghanistan kwa kuzingatia nafasi ya Russia na China ambazo ni nchi mbili muhimu duniani.  

 

Tags