Oct 14, 2021 12:58 UTC
  • Rais wa Russia: China haihitaji kutumia nguvu za kijeshi ili kuungana tena na Taiwan

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema, chaguo la kijeshi halihitajiki kuwa mbadala wa njia ya amani ili kuiwezesha China kuungana na Taiwan.

Putin ameyasema hayo katika mkutano wa Wiki ya Nishati ya nchi hiyo uliofanyika mjini Moscow na kusisitiza kuwa, China haihitaji kutumia mabavu kwa ajili ya kufikia kwenye umoja na muungano inaoutaka na Taiwan.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo, Rais wa Russia amesema, nafasi ya sarafu ya dola ya Marekani duniani inaendelea kulegalega kutokana na sera mbovu na zisizo sahihi za nchi hiyo.

Putin ameongeza kuwa, kiwango cha matumizi na cha akiba ya dola ya Marekani cha nchi mbalimbali duniani kinaendelea kupungua.

Katika mkutano uliojumuisha ndani yake masuali kutoka kwa waandishi wa habari, rais wa Russia alikataa kujibu suali aliloulizwa kuhusu msimamo wake wa kugombea au kutogombea katika uchaguzi ujao wa rais wa nchi hiyo.

Uchaguzi wa rais wa Russia utafanyika Machi 2024 na kwa mujibu wa mabadiliko iliyofanyiwa katiba ya nchi hiyo, Putin anaweza kuwania tena urais kwa muhula mwingine.

Vladimir Putin amekuwa rais wa Russia tangu mwaka 2000; na ni katika kipindi kimoja tu cha 2008 hadi 2012 alishika wadhifa wa uwaziri mkuu wa nchi hiyo.../

Tags