Oct 14, 2021 13:05 UTC
  • Waziri wa zamani wa Uingereza: Kuondolewa vikwazo ni takwa halali kisheria la Iran

Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Uingereza, amesema kuhusu msimamo wa Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA ya mjini Vienna, wa kutaka iondolewe vikwazo vyote vya kidhalimu iliyowekewa na Marekani kwamba, kuondolewa vikwazo hivyo ni takwa halali kisheria la Tehran.

Jack Straw amekiri kuwa, hatua ya upande mmoja iliyochukuliwa na serikali iliyopita ya Marekani ya Donald Trump ya kujitoa kwenye JCPOA ndio chanzo kikuu cha matatizo ya sasa; na akasisitiza kuwa yeye anataka Marekani iondoe vikwazo ilivyoiwekea Iran.

Straw ameeleza kwamba, msimamo wa Marekani wa kujivutia upande wake na kutaka iwe na upendeleo zaidi kuhusiana na mazungumzo ya Vienna kwa ajili ya kuondoa vikwazo, sambamba na kutaka kuingiza masuala mengine katika mazungumzo hayo, ni mtazamo wenye utata na usioendana na uhalisia.

Kauli hiyo ya waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Uingereza, imetolewa sambamba na safari ya Enrique Mora, mwakilishi wa Umoja wa Ulaya wa Sera za Kigeni na za Usalama hapa mjini Tehran.

Ali Bagheri, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuhusu safari hiyo ya Mora na kueleza kwamba, "leo Alkhamisi nitakuwa mwenyeji wa Enrique Mora, katika mwendelezo wa mashauriano ya karibuni ya kikanda na kimataifa".

Bagheri ameongeza kuwa, kubadilishana mawazo juu ya masuala ya pande mbili na ya kikanda ikiwemo Afghanistan na vilevile kuzungumzia namna ya kuondolewa vikwazo vya kidhalimu ndizo ajenda zitakazojadiliwa katika safari hiyo.

Hadi sasa zimeshafanyika duru sita za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja baina ya Marekani na pande zilizosalia katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ili kurahisisha na kufungua njia kwa Washington ya kurudi kwenye makubaliano hayo.../

Tags