Oct 15, 2021 09:16 UTC
  • Onyo la Putin kuhusu kuhamishiwa ugaidi nchini Afghanistan

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema magaidi wanahamishwa kutoka Iraq na Syria na kupelekwa Afghanistan jambo ambalo amesisitiza kuwa linahatarisha usalama wa nchi za Umoja wa Sovieti ya zamani.

Kwa msingi huo amesisitiza juu ya udharura wa kuimarishwa usalama katika mipka ya nchi hizo na Afganistan na kutaka askari usalama na polisi katika mipaka hiyo wawe macho kwa ajili ya kutekeleza operesheni maalumu za pamoja kwa lengo la kukabiliana na tishio la magaidi hao.

Akizungumza wiki iliyopita, Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia alisema nchi yake ina wasi wasi kuhusiana na kuongezeka magaidi wa kundi la Daesh katika ardhi ya Afghanistan. Baada ya Taliban kudhibiti Afghanistan, magaidi wa Daesh wameimarisha operesheni zao za kigaidi katika nchi hiyo kama tulivyoona wakijilipua katika misikiti miwili muhimu huko Kabul na katika wilaya ya Kunduz. Katika siku za karibuni ripoti za kuaminika zimekuwa zikitolewa kuhusu kuhamishiwa Afghanistan magaidi wapya wa kundi hilo kutoka katika nchi za Iraq na Syria.

Maria Zakharova

Suala hilo limeongeza wasi wasi wa Russia na nchi za Asia ya Kati kwa kutilia maanani kuwa kuongezeka shughuli za kigaidi za Daesh huko Afghanistan kunaweza kurahisisha upenyaji wa magaidi hao katika nchi za Asia ya Kati na hatimaye kuingia Russia.

Baada ya kuondoka kwa fedheha askari wa Marekani huko Afghanistan, Washingtton ilitaka kutumia vituo vya kijeshi vya nchi za Asia ya Kati kwa ajili ya kukabiliana na kile kilichodaiwa kuwa ugaidi katika ardhi ya Afganistan lakini jambo hilo lilipingwa vikali na Moscow pamoja na nchi za Asia ya Kati. Viongozi tofauti wa Russia wakiwemo mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi wa nchi hiyo walipinga kutumiwa vituo vya kijeshi vya nchi za Asia Magharibi kwa ajili ya shughuli za kijeshi za Marekai na kusema jambo hilo lingehatarisha usalama wa nchi za eneo.

Viongozi wa kisiasa na kiusalama wa Russia wanasema Marekani yenyewe ndiyo msababishaji mkuu wa hali ya kusikitisha ya Afghanistan na uwepo wa magaidi katika nchi hiyo, na hasa hivi sasa ambapo inahamishia huko magaidi wa Daesh kutoka Iraq na Syria hivyo haifai kudai kuwa inataka kupambana na magaidi hao.

Rustam Minkayev, mmoja wa makamanda wa Russia alisema mwanzoni mwa mwezi Oktoba kwamba wana ripoti zinazothibitisha kuwa magaidi wa Daesh wanahamishwa kutoka maeneo yanayodhibitiwa na Marekani huko Syria na Iraq na kupelekwa Afghanistan.

Rustam Minkayev

Kamanda huyo anaendelea kusema kwamba askari maalumu wa Marekani wanaendelea kujishughulisha na uhamishaji huo wa magaidi wa Daesh kuelekea Afghanistan na hasa katika meneo ya kaskazini mwa nchi hiyo jambo ambalo anasema bila shaka tulivuruga usalama wa nchi jirani.

Marekani daima imekuwa ikitumia magaidi wa Daesh dhidi ya washindani wake na hasa Russia na China na kwa kuzingatia uwepo wa mpaka wa pamoja kati ya Afghanistana na China na vilevile nchi za Asia ya Kati, bila shaka kutumiwa Daesh na kuhamishiwa magaidi hao huko Afghanistan kunatekelezwa kwa ajili ya kutoa mashinikizo dhidi ya Russia na China na hivyo kuhatarisha usalama wazo.

Tags