Oct 15, 2021 14:05 UTC
  • Instagram yafunga ukurasa wa Press TV katika ukiukaji uhuru wa maoni

Shirika la Kimarekani la mtandao wa kijamii wa Instagram limefunga ukurasa wa televisheni ya kimataifa ya Iran ya Press TV ikiwa ni katika hujuma nyingine ya mashirika ya mitandao ya kijamii ya Marekani dhidi ya vyombo vya habari vya Iran.

Kitengo cha mitandao ya kijamii katika Press TV kimetangaza kuwa akaunti ya Instagram yenye anwani ya https://www.instagram.com/presstvchannel  imefungwa tokea Oktoba 8 kwa sababu zisizojulikana.

Wakati ambao  Shirika la Facebook linalomiliki Instagram limesema litatuma kile ambacho limedai ni ‘nambari ya siri’ ili kufungua akaunti hiyo, hadi sasa Press TV haijapokea nambari hiyo.

Press TV ilijiunga na Instagram mwaka 2015 na imekuwa ikituma picha na video za habari ambapo hujikita zaidi na taarifa ambazo haziripotiwi au zinazofichwa na vyombo vingine vya habari duniani.

Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani, kwa mara kadhaa imechukua hatua dhidi ya vyombo vya habari vya Iran hasa Press TV, ambapo akaunti zake za Twitter, Facebook, Instagram na Gmail zimefungwa.

Ingawa mashirika ya mitandao ya kijamii Marekani hudai kuwa vyombo vya habari vya Iran vimekiuka kanuni, lakini wakati huo huo mashirika hayo ya mitando ya kijamii huwapa jukwaa wale wenye chuki dhidi ya Uislamu na Iran kwa kisingizio cha ‘uhuru wa maoni’ na  nukta hii ni ishara ya wazi ya undumakuwili.

Mwezi Juni mwaka huu Idara ya Mahakama Marekani iliteka tovuti 33 za Jumuiya ya Radio na Televisheni za Kiislamu kama vile PressTV, Al Alam na Alkauthar za Iran, Al Masirah ya Yemen na Lualua ya Bahrain. Tovuti za Iran zilizofungwa zilikuwa zina domain inayoishia na kikoa cha .com na sasa inapatikana kupitia .ir.