Oct 16, 2021 02:32 UTC
  • Mbunge wa chama tawala Uingereza auawa kwa kisu kanisani

Mbunge mmoja wa chama tawala cha kihafidhina nchini Uingereza ameuawa kwa kuchomwa kisu kanisani na mtu asiyejulikana katika mji wa Leigh-on-Sea kusini mwa nchi.

David Amess aliyekuwa mwakilishi wa eneo la Southend West katika jimbo la Essex, kusini mashariki mwa Uingereza aliuawa jana Ijumaa, baada ya kuchomwa kisu shingoni alipokuwa anazungumza na wapigakura katika Kanisa la Kimethodisti la Belfairs katika mji wa Leigh-on-Sea.

Taarifa ya polisi ya Uingereza imesema Sir David Amess aliyekuwa na umri wa miaka 69, aliaga dunia katika eneo la tukio, licha ya jitihada za madaktari za kujaribu kuyaokoa maisha yake.

Mwanasiasa huyo amekuwa mbunge wa chama cha Conservative cha Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johson tokea mwaka 1983.

Kijana wa miaka 25 anayetuhumiwa kuhusu na mauaji hayo amekamatwa na maafisa wa polisi, huku uchunguzi wa mauaji hayo yaliyofanyika mchana kweupe ukiendelea.

Polisi ya Uingereza imesema haifanyi msako wa kutafuta washukiwa zaidi wa mauaji hayo, ikisisitiza kuwa ishara zote zinaashiria kuwa kijana aliyekamatwa ndiye aliyehusika na ukatili huo.

 

Tags