Oct 16, 2021 12:04 UTC
  • Mlipuko katika msikiti wa Washia katika mji wa Qandahar, Afghanistan

Makumi ya watu waliokuwa katika Swala ya Ijumaa wameuawa shahidi na wengine karibu ya mia moja wamejeruhiwa katika milipuko miwili iliyotokea jana Ijumaa katika Msikiti wa Bibi Fatima katika mji wa Qandahar Afghanistan. Hii ni mara ya pili kwa Msikiti wa Washia kukumbwa na milipuko huko Afghanistan katika muda wa wiki moja.

Mamia ya watu waliuawa na kujeruhuhiwa pia katika mlipuko Ijumaa iliyopita walipokuwa katika Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Washia huko Kunduz Afghanistan. Mlipuko wa jana Ijumaa umetokea katika hali ambayo kundi la Taliban ndilo linaloongoza huko Afghanistan; na baada ya mlipuko wa Kunduz liliahidi kuwa jinai kama hiyo haingekaririwa tena nchini humo na kwamba lina uwezo wa kuwadhaminia usalama wananchi wa Afghanistan khususan Waislamu wa Kishia. Taliban hivi sasa inakabiliwa na changamoto ya mashambulizi katika hali ambayo kundi hilo pia lilikuwa likitekeleza mashambulizi kama hayo katika utawala  wa zamani nchini humo; na sasa kundi linaloipinga Taliban kwa jina la Daesh linaendesha harakati na hujuma dhidi ya kundi hilo na wananchi wa Afghanistan. Hii ina maana kuwa, kundi la Taliban linajua vyema namna mashambulizi hayo yanavyotekelezwa na linaweza kuyadhibiti mara moja. Kwa msingi huo kukaririwa mashambulizi  ya kigaidi kama hayo katika Msikiti wa Washia ni jambo lenye kutia shaka. 

Jinai ya magaidi katika Msikiti wa Washia huko Qandahar, Afghanistan 

Frans Elias mchambuzi wa masuala ya kisiasa huko Lebanon anaamini kwamba: Taswira halisi kuhusu usalama wa Afghanistan haifahamiki, sawa kabisa na kama ambavyo Marekani ilivyogonga mwamba huko Afghanistan baada ya kuwepo kwa miongo miwili nchini humo. Kwa hiyo njia pekee ya kutatua mgogoro wa Afghanistan ni kufikiwa mapatano ya kitaifa.  

Makundi ya kigaidi yamekuwa changamoto na kuchagiza uwezo wa kudhamini usalama wa kundi la Taliban na hivyo kushuhudiwa mlipuko huo tajwa huko Qandahar inayohesabiwa kuwa ngome ya jadi ya kundi la Taliban. Kitendo cha  magaidi cha kuwauwa  Washia huko Qandahar si tu ni jambo lenye kuitia Taliban wasiwasi mkubwa kwa upande wa itabari, bali kivitendo magaidi wameonyesha uwezo wao wa kushambulia ngome ya kundi Taliban; jambo ambalo linaweza kuibua wasiwasi pia kwa wananchi wa mji huo. Kwa msingi huo, swali hili muhimu linaulizwa kwamba je, Taliban katika muda wa wiki moja iliyopita yaani baada ya shambulio la kigaidi huko Kunduz imechukua hatua gani za kiusalama na zinazofaa kuwadhaminia usalama wananchi wa Afghanistan? Hata kama Taliban kidhahiri imeonyesha msimamo wa kati na kati kuhusu kuuliwa Washia lakini hakuna shaka kuwa magaidi wanastafidi na mianya ya ukosefu wa usalama ili kuhatarisha maisha ya wananchi wote wa Afghanistan. 

Magaidi wa Daesh Afghanistan 

Abdulbasit mtafiti katika Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti ya Rajaratnam huko Singapore anaamini kuwa kuendelea mashambulizi ya kigaidi huko Afghanistan kunaonyesha kuwa hakuna kundi linaloweza kudai kuwa na uwezo wa kudhamini usalama nchini humo; au kudai kushikilia madaraka huko Afghanistan; na ndio maana Taliban inapitia wakati mgumu sana hivi sasa.   

Ala kul haal, kitendo cha kundi la Taliban cha kulaani kidhahiri tu jinai za magaidi ni kukaririwa tu matukio ya umwagaji damu ya wakati wa utawala wa Rais Ashraf-Ghani ambayo yalikuwa yakifanywa huko Afghanistan na Taliban yenyewe na makundi mengine yanayozusha machafuko; vitendo ambavyo vilikuwa vikilaaniwa pia na viongozi wa serikali ya zamani ya nchi hiyo. Kwa msingi huo, si jambo lililo mbali kuwa na mkono mabaki ya idara za intelijinsia za serikali liyopita katika kuuawa wananchi madhali Taliban imeshindwa kuchukau hatua za kuunda serikali shirikishi kwa kuyajumuisha makundi mbalimbali ya kikaumu na kimadhehebu katika muundo wa serikali ya Afghanistan.

Ashraf-Ghani, Rais wa Afghanistan aliyekimbia nchi 

 

Tags