Oct 17, 2021 02:25 UTC
  • Kurejea Marekani katika Baraza la Haki za Binadamu la UN; shaka na shubha kuhusu suala hilo

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa juzi Alhamisi liliiarifisha Marekani kuwa moja kati ya wanachama 18 wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Duru ya miaka mitatu ya baraza hilo itaanza kuanzia Januari Mosi mwaka ujao wa 2022. Nchi wanachama wa baraza hilo huchaguliwa katika kila duru katika upigaji kura unaofanyika kwa njia ya siri.

Katika duru ya sasa Marekani imekuwa moja ya nchi wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu kwa kupata kura 168 za ndio kati ya kura zote 193 zilizopigwa. Mwaka 2018 Marekani ilijitoa katika taasisi hiyo ya kimataifa kwa kudai kuwa imekuwa ikizipendelea nchi nyingine mkabala wa utawala wa Kizayuni. Kwa utaratibu huo, Marekani kwa mara nyingine tena imejiunga na Baraza la Haki za Binadamu la UN baada ya kupita miaka mitatu na nusu tangu serikali ya zamani ya  Marekani chini ya uongozi wa Rais Donald Trump ijitoe kwa upande mmoja katika baraza hilo. 

Rais wa sasa wa Marekani Joe Biden aliahidi baada ya kuingia White House mwezi Januari mwaka huu kwamba atabadili maamuzi na hatua zilizochukuliwa na Trump na kuirejesha Marekani katika taasisi na makubaliano mbalimbali ya kimataifa ambayo serikali ya Trump ilitangaza kuindoa nchi hiyo. Moja ya taasisi hizo ilikuwa ni Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa; na serikali ya Biden sasa imetekeleza ahadi yake baada ya kuichelewesha kwa miezi kumi. Hata hivyo tunapasa kuona iwapo Washington itakuwa tayari kutambua rasmi masuala mengi ya ukiukaji wa haki za binadamu unaoshuhudiwa ndani ya Marekani kwenyewe na kuchukua hatua kutatua masuala hayo licha ya madai chungu nzima ya serikali ya Biden kuhusu haki za binadamu na  kuunga mkono  kile kinachoonekana sasa kama ukosoaji  na kuziwekea vikwazo nchi kinzani na mahasimu wake kama China na Russia au la.  

Rais Joe Biden wa Marekani  

Kabla ya hapo, Baraza la Haki za Binadamu la UN liliashiria katika ripoti yake masuala mengi ya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Marekani kama vile ubaguzi mkubwa wa rangi, ukiukaji wa haki za wafungwa, kukiukwa haki za wenyeji asilia wa Marekani, ukiukaji wa haki za wanawake, kukandamizwa wahajiri haramu na wakimbizi na mengineyo na kutaka kukomeshwa visa hivyo. Khususan Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilikosoa hali mbaya na isiyo ya kibinadamu ya raia weusi na ubaguzi wa kimfumo nchini Marekani na kutaka kutekelezwa mabadiliko. Haya yote yanashuhudiwa katika nchi ambayo inadai kuwa mshika bendera na mtetezi wa haki za binadamu duniani. Si hayo tu bali siku zote Marekani imekuwa ikipuuza matakwa ya Baraza la Haki za Binadamu.   

Sara Fallahi Mjumbe wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran anasema: Marekani inatumia mbinu mbalimbali kuingilia masuala ya nch nyingine; na kuandaa uwanja wa kuziondoa madarakani serikali mbalimbali duniani kwa kisingizio cha kujenga demokrasia na kupambana na udikteta; katika hali ambayo yenyewe inakabiliwa na migawanyiko anuwai ya kitabaka, kijinsia, kitaifa na kiuchumi. 

Sara Fallahi, Mjumbe wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran

Jambo jingine ni kuwa, serikali ya Biden ilipoingia madarakani iliahidi kuwa itatazama upya uhusiano kati yake na nchi waitifaki wa Washington ambazo zinakiuka haki za binadamu khususan Saudi Arabia. Utawala wa Saudia si tu unakiuka wazi haki za raia wa nchi hiyo ndani ya Saudia tu bali tangu mwaka 2015 nchi hiyo pamoja na Imarati zimeanzisha vita vya kidhalimu dhidi ya Yemen na kuua maelfu ya raia wa nchi hiyo katika mashambulizi yao makubwa ya anga. Nchi hizo  zimebomoa na kuharibu pakubwa pia miundombinu ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Wakati huo huo licha ya taasisi za kutetea haki za binadamu duniani kulaani mara kadhaa jinai za muungano vamizi dhidi ya Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia lakini Marekani na waitifaki wa Ulaya wana nafasi kuu na kubeba dhima katika kuzipatia Saudia na Imarati silaha, misaada ya kilojistiki na kiintelijinsia ili kuendeleza mashambulizi dhidi ya Yemen. Akiwa katika kampeni za uchaguzi Joe Biden alipiga nara na shaari dhidi ya Riyadh na kuvitaja vita vya Yemen kuwa "Janga la Kimkakati". Aidha alidai kuwa angehitimisha oparesheni za mashambulizi ya muungano wa Saudia huko Yemen kwa uungaji mkono wa Marekani ikiwemo uuzaji wa silaha kwa nchi hiyo. Pamoja na hayo lakini Joe Biden kwa mara nyingine aliitaja Saudi Arabia kuwa muitifaki wa karibu wa Marekani mara baada ya kuingia White House; na kuanzisha tena miamala ya silaha na Saudia na Imarati. Swali linaloulizwa sasa ni kwamba je, Marekani kwa kuwa mwanachama tena wa Baraza la Haki za Binadamu la UN, imedhamiria kurekebisha na kufuta makosa yake au inataka tu kuitumia taasisi hiyo ya haki za binadamu kama wenzo wa kutimiza maslahi yake? 

Madhara ya vita vya Saudia na waitifaki wake huko Yemen 

 

Tags