Oct 17, 2021 02:26 UTC
  • Jumuiya ya Kutetea Wahanga wa Ugaidi: Ugaidi unatumiwa kulinda maslahi ya madola ya kibeberu

Jumuiya ya Kutetea Wahanga wa Ugaidi yenye makao yake nchini Iran imetangaza kuwa, ugaidi umekuwa ukitumiwa kama fimbo na wenzo wa kulinda na kupanua maslahi ya madola ya kibeberu na wala hauna mfungamano na dini wala madhehebu yoyote ya dini.

Taarifa ya jumuiya hiyo imetolewa kulaani shambulizi la kigaidi lililolenga Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Bibi Fatima katika mji wa Kandahar nchini Afghanistan. Taarifa hiyo imesema kuwa, mashambulizi yanayofanyika dhidi ya misikiti, makanisa na nyumba nyingine za ibada katika miaka ya karibu yamethibitisha kuwa ugaidi unatumiwa kama wenzo wa kudhamini maslahi ya madola makubwa ya kibeberu na wala hauna mfungamano wowote na dini au madhehebu makhsusi, na kinyume chake, dini za Mwenyezi Mungu na wafuasi wa dini hizo ndio wanaolengwa zaidi kwa mashambulizi ya magaidi, magenge ya kitakfiri na yale yenye misimamo ya kuchupa mipaka. 

Jumuiya ya Kutetea Wahanga wa Ugaidi imehoji kuwa, kuua watu wanaofanya ibada msikitini kuna thamani au fahari gani? 

Zaidi ya Waislamu 60 wameuawa katika Swala ya Ijumaa Kandahar

Zaidi ya Waislamu sitini wa madhehebu ya Shia waliuawa shahidi wakati milipuko mitatu ilipoulenga msikiti wa Bibi Fatima kwenye Swala ya Ijumaa wiki hii huko Kandahar.

Kundi la kigaidi la ISIS-K au Daesh limedai kuhusika na hujuma hiyo. 

Wiki iliyopita pia Waislamu wasiopungua mia moja waliuawa katika shambulizi la kigaidi lililolenga waumini waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa katika mji wa Kunduz nchini Afghanistan na wengine karibu mia mbili wamejeruhiwa. 

Shambulizi hilo lililenga msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika eneo la Khan Abad na lilifanywa na kundi hilo hilo na mawahabi la Daesh (ISIL-K).

Tags