Oct 17, 2021 08:07 UTC
  • Azma ya Iran na China ya kutekeleza Mapatano ya Miaka 25

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Watu wa China wamefanya mazungumzo ya simu na kusisitiza kuwa nchi mbili hizi zina azma ya kutekeleza 'Mapatano ya Miaka 25.'

Katika mazungumzo hayo, Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema uhusiano  wa nchi hizi mbili ni wa kistratijia na kuongeza kuwa Iran inalipa uzito mkubwa suala la kufuatilia utekelezaji kikamilifu 'Mapatano ya Miaka 25' ya ushirikiano wa pande mbili.

Kwa upande wake, Wang Yi Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesema hali ya kieneo na dunia imebadilika na hivyo Beijing inajitayarisha kuimarisha uhusiano wake wa kistratijia na Iran.

Ameongeza kuwa China inataka kushirikiana na Iran katika kupinga utumiaji mabavu na kutetea usawa na uadilifu katika uga wa kimataifa.

 Hossein Amir-Abdollahian (kushoto) na Wang Yi

Mnamo Machi 27 mwaka huu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Watu wa China zilitiliana saini hati ya  ushirikiano wa pande zote ambayo ni maarufu kwa  jina la "Hati ya Miaka 25".

Hati hii inahusu ushirikiano wa muda mrefu baina ya nchi hizi mbili katika nyuga za siasa, uchumi, utamaduni na masuala ya kistratijia.

Uhusiano baina ya Iran na China ni wa kihistoria na umekuwepo kwa muda mrefu na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu uhusiano wa nchi mbili uliingia katika duru mpya.

China na Iran kama madola mawili makubwa na yenye nguvu katika eneo na dunia yamearifisha uhusiano mpya wa pande mbili katika nyanja  zote na pia uhusiano wa pande kadhaa katika taasisi za kimataifa kama vile Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai. Kwa hivyo uhusiano wa China na Iran unadhamini maslahi ya pande mbili.

China daima imekuwa ikiunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA na imeitaka serikali ya Marekani iondoe vikwazo vyote vya upande mmoja dhidi ya Iran bila masharti.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo pia imepinga uingiliaji wa madola ya Magharibi hasa Marekani katika mambo ya ndani ya China kuhusiana na kadhia za Hong Kong, Taiwan na kusema kadhia hizo ni masuala ya ndani ya China.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano wake na Rais wa China Xi Jinping aliyekuwa safarini Tehran Januari 2016 aliashiria siasa za kibeberu za baadhi ya nchi hususan Marekani na ushirikiano wao usio na mwamana na nchi nyingine na kuongeza kuwa: "Jambo hilo limezifanya nchi huru kupanua zaidi ushirikiano baina yao na makubaliano ya Iran na China ya kuwa na uhusiano wa kiistratijia wa miaka 25 yamefikiwa katika fremu hiyo hiyo na kwa hakika inabidi pande mbili zilipe uzito mkubwa suala la kufuatilia makubaliano hayo na kuyaingiza kwenye hatua za utekelezaji."

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu (kulia) katika mkutano na Rais wa China Xi Jinping 

Mbali na misimamo ya pamoja ya Iran na China katika masuala mengi ya kisiasa na kiusalama, ikiwa  ni pamoja na kupinga hatua za upande mmoja za Marekani katika eneo, uhusiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya Iran na China ni jambo lenye umuhimu mkubwa. Hivi sasa China imewekeza kwa kiasi kikubwa katika mradi wa uchukuzi unaojulikana kama 'Ukanda Mmoja, Njia Moja' ambao unahusisha makumi ya nchi duniani. Mradi huu kimsingi ni njia za nchi kavu na baharini ambazo zitatumika kuunganisha nchi husika na Iran ni moja ya nchi muhimu zaidi katika mradi huo; kimsingi Iran sasa ni daraja la kuunganisha nchi za bara Asia na Ulaya.

Aidha kutokana na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi, Iran inakidhi kwa kiasi kikubwa mahitaji ya nishati ya China na uhusiano katika nyanja hii unaimarika.

Hakuna shaka kuwa matukio ya kimataifa, hasa ustawi wa uchumi wa bara Asia na sera za nchi kama Iran za kuimarisha uhusiano na bara Asia ni jambo ambalo litapelekea bara hili kuwa kitovu kikuu cha uwekezaji duniani.

Ni kwa msingi huu ndio wakuu wa Iran na China wakasisitiza ulazima wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kwa hivyo katika mazungumzo ya Ijumaa mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na China walisisitiza kuhusu kutekeleza 'Hati ya Miaka 25' ya ushirikiano wa pande mbili.

 

Tags