Oct 18, 2021 12:22 UTC
  •  New York Times: Chama tawala India kinawafukuza Waislamu eneo la Assam

Gazeti la The New York Times limefichua kwamba chama tawala nchini India cha Bharatiya Janata Party (BJP) kimeanzisha kampeni ya kuwafukuza Waislamu wakazi asili wa jimbo la Assam kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Ripoti iliyotayarishwa na gazeti hilo imeonesha picha za video za vurugu na kuchomwa moto nyumba za Waislamu katika jimbo hilo ikiwa ni katika kampeni ya serikali ya kuwafurusha kwa nguvu katika eneo hilo linalopakana na Bangladesh.

Maafisa wa serikali za mitaa nchini India wamehalalisha kampeni hiyo wakidai kuwa inalenga idadi kubwa ya wahamiaji haramu kutoka Bangladesh ambao wanaishi kwenye ardhi ya miradi muhimu ya kilimo.

Hata hivyo nyaraka rasmi na mahojiano kadhaa yaliyofanywa na gazeti New York Times yameonyesha kuwa wakazi wengi waliofukuzwa ni raia halali wenye haki ya kuishi kwenye ardhi inayomilikiwa na serikali. Vilevle wakosoaji wa serikali ya India wanasema kufukuzwa kwa Waislamu hao katika jimbo la Assam ni sehemu ya kampeni pana ya chama tawala dhidi ya Waislamu kote nchini India.

Gazeti hilo linasisitiza kwamba Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi na chama chake tawala cha Bharatiya Janata wamefanikiwa kuhamasisha kambi yao ya kitaifa ya Uhindu kuunga mkono mipango inayowakandamiza Waislamu zaidi ya milioni 200 wa nchi hiyo.

Mwezi Disemba 2019, India ilipitisha sheria ya uhamiaji ambayo inaharakisha utoaji wa uraia kwa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani ikiwa tu ni Wahindu au wa imani zingine, isipokuwa Waislamu.

Mwishoni mwa mwaka uliopita pia shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilisema jeshi la polisi la India ilifanya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kwa kushirikiana na magenge ya Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mipaka kuwashambulia Waislamu katika mji mkuu New Delhi mapema mwaka huu.

Wahindu wakiwatesa Waislamu, India

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita zimeshuhudiwa hatua na maamuzi kadhaa yaliyochukuliwa na serikali ya India dhidi ya Waislamu, ambayo yamezusha malalamiko makubwa ndani na nje ya nchi hiyo.

Kuwapatia Wahindu ardhi ya msikiti wa kihistoria walioubomoa wa Babri, kufutwa mamlaka maalumu ya ndani ya kujiendeshea mambo yake liliyokuwa limepewa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India ambalo wakazi wake ni Waislamu, kubatilishwa uraia wa mamia ya maelfu ya Waislamu, kupitishwa sheria mpya ya uraia na kuwapatia uraia wa India raia wa kigeni kwa sharti la kutokuwa Waislamu, ni baadhi tu ya maamuzi ya kibaguzi yaliyochukuliwa na serikali ya chama tawala cha Kihindu cha Bharatiya Janata (BJP) nchini India dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.