Oct 18, 2021 14:09 UTC
  • Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani afariki dunia akiwa na umri wa miaka 84

Colin Powell, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani wakati wa urais wa George Bush mwana, na Mkuu wa Majeshi ya Marekani wakati wa urais wa George Bush baba, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 84 kwa matatizo ya corona.

Kanali ya televisheni ya CNN imenukuu taarifa iliyotolewa na familia yake ikisema kuwa, Powell amefariki dunia kwa ugonjwa wa UVIKO-19 licha ya kwamba alikuwa amepiga dozi zote mbili za chanjo ya corona ya Pfizer ya Marekani.

Powel alikuwa waziri wa kwanza wa mambo ya nje wa Marekani mwenye asili ya Afrika aliyehudumu kwenye serikali kadhaa za marais wa Republican tangu ulipokuja mfumo mpya wa siasa za mambo ya nje wa White House ulioanza mwishoni mwa karne ya 20 na mwanzoni mwa karne ya 21. 

Powell akitoa ushahidi wa uongo kuhusu silaha za Iraq mbele ya Baraza la Usalama, mwaka 2003

 

Kuanzia mwezi Oktoba 1989 hadi Septemba 1993, Powell alihudumu kama mkuu wa 12 wa majeshi ya Marekani. Katika kipindi hicho alishiriki kwenye migogoro 28 iliyoanzishwa na Marekani likiwemo shambulio la nchi hiyo huko Panama mwaka 1989 na Opresheni ya Kimbunga cha Jangwani ya kumtoa Saddam Hussein nchini Kuwait katika miaka 1990 na 1991.

Tarehe 5 Februari 2003, wakati akiwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Colin Powell alihutubia Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na kutetea vikali vita vya kijinai vya marekani na kundi lake nchini Iraq.

Katika hotuba yake hiyo, Powell alitoa ushahidi wa uongo mbele ya Baraza la Usalama akidai kuwa hana shaka hata kidogo kwamba Saddam alikuwa anamiliki silaha hatari za biolojia na nyuklia na ana uwezo wa kuzalisha kwa wingi na haraka silaha hizo. Hata hivyo tarehe 13 Septemba 2004 Powell alikiri hadharani kuwa nyaraka alizopewa na CIA zilikuwa za uongo na kwamba hakukuwa na silaha za mauaji ya umati huko Iraq.