Oct 19, 2021 07:41 UTC
  • Mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Afghanistan ajiuzulu

Zalmay Khalilzad, anayetazamwa kama nembo na kielelezo kikubwa zaidi cha kufeli kidiplomasia Marekani nchini Afghanistan amejiuzulu wadhifa wake wa mjumbe maalumu wa Washington katika masuala ya nchi hiyo.

Baada ya Khalilzad kuchukua uamuzi wa kujiuzulu wadhifa wake huo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alimtangaza Tom West kuwa mwakilishi mpya maalumu wa nchi hiyo katika masuala ya Afghanistan.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Zalmay Khalilzad ametetea rekodi ya utendaji wake, lakini amekiri pia kwamba katika jukumu lake la mwisho alilokabidhiwa hakuweza kupata lile alilokuwa akilitaka na kwamba mahusiano ya kisiasa baina ya serikali ya Afghanistan na Taliban hayakuwa kama walivyokuwa wameyapanga yawe.

Khalilzad (kushoto) na mwakilishi wa Taliban wakisaini makubaliano ya suluhu Doha, Qatar

Kwa muda wa miaka mitatu ya kuhudumu kama mjumbe maalumu wa Marekani katika masuala ya Afghanistan, Zalmay Khalilzad aliongoza mazungumzo baina ya Washington na kundi la Taliban na ndiye aliyekuwa na nafasi kuu katika mazungumzo hayo ya kufikia suluhu na kundi hilo.

Baada ya miaka 20 ya kuivamia kijeshi na kuikalia kwa mabavu Afghanistan, hatimaye mnamo mwishoni mwa mwezi Agosti, Marekani iliondoka nchini humo ikiwa imeshindwa kwa namna ya kuaibisha na kudhalilisha.../

Tags