Oct 19, 2021 07:44 UTC
  • Biden apewa ushauri hatari wa kupeleka mabomu ya atomiki Taiwan ili kukabiliana na China

Taasisi moja ya wanafikra wenye misimamo ya kufurutu mpaka nchini Marekani imeeleza katika andiko lake moja la upembuzi kwamba, kuna ulazima kwa serikali ya Marekani kuweka mabomu ya atomiki katika kisiwa cha Taiwan ili kukisaidia kisiwa hicho dhidi ya China.

Taasisi ya Gatestone imeeleza katika uchambuzi wake huo kuwa, Rais Joe Biden wa Marekani anaweza kurejesha tena mkakati wa kuzuia hujuma za mashambulio kwa kupendekeza mkataba wa ulinzi baina ya Washington na Taiwan.

Sehemu nyingine ya uchambuzi huo wa Gatestone imeeleza kuwa, ikiwa yeye Biden hataki kufanya hivyo, itapasa aanzishe vituo maalumu vya silaha za atomiki ndani ya Taiwan au kuhamishia silaha hizo katika kisiwa hicho ili kiweze kujilinda.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo yenye misimamo ya kufurutu ada, baada ya kutekwa mji mkuu wa Afghanistan Kabul, Taiwan sasa ni mtihani wa kuipima azma ya Marekani, kwa hivyo Washington inapasa ichukue hatua zisizo za kawaida kwa ajili ya kukilinda kisiwa hicho.

Hayo yanaripotiwa huku uchambuzi mwingine uliofanywa na chaneli ya habari ya Russia Today ukieleza kwamba, ikiwa China itaamua kuishambulia kijeshi Taiwan, lazima itakuwa imeshaufanyia tathmini pana na ya kina ya kiintelijensia uwezekano wa kufanikiwa na kutoka na ushindi katika shambulio hilo.

Duru za habari ziliripoti siku ya Jumamosi kuwa,Taiwan inafuatilia uwezekano wa kupokea kabla ya muda ulioafikiwa ndege 66 za kivita aina ya F-16 na zaidi ya makombora 100 ya masafa ya mbali aina ya AGM-158 kutoka Marekani yenye uwezo wa kushambulia ardhi ya China.../