Oct 19, 2021 13:06 UTC
  • Kuongezeka mizozo na mivutano baina ya Russia na NATO

Sambamba na kuongezeka mIzozo na mivutano baina ya Russia na Shirika la Kijeshi la NATO, serikali ya Moscow imetangaza kuwa, itakata uhusiano wake na shirika hilo.

Sergei Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia ametangaza kuwa, kuanzia mwezi ujao wa Novemba, nchi hiyo itakataka kikamilifu uhusiano wake wa kidiplomasia na NATO na kwamba, ofisi ya shirika hilo itafungwa. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa  Russia amesisitiza kuwa, kama NATO inataka mazungumzo, inaweza kufanya mazungumzo na balozi wa Russia nchini Ubelgiji.

Hatua hii ya Russia imechukuliwa katika hali ambayo, wiki mbili zilizopita Shirika la Kijeshi la NATO liliwafukuza wanadiplomasia wanane wa Russia kutoka katika makao makuu ya shirika hilo. Katika kuhalalisha kitendo hicho, NATO ilitangaza kuwa, wanadiplomasia hao wanane walikuwa wakifanya mambo ya siri katika kalibu ya maafisa wa masuala ya kiintelijensia; madai ambayo yamekanushwa vikali na serikali ya Moscow. Leonid Slutsky, Mkuu wa Kamisheni ya Masuala ya Kimataifa ya Bunge la Russia (DUMA) amekosoa vikali uamuzi huo wa NATO wa kuwafukuuza wanadiplomasia wa Russia na kueleza kwamba, madai yaliyotolewa na shirika hilo hayana msingi wowote kama ambavyo hakuna nyaraka wala ushahidi uliotolewa wa kuthibitisha madai hayo.

Mikhail Shinkaman mweledi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa sanjari na kuashiria uamuzi wa kufukuzwa wafanyakazi wa ofisi ya uwakilishi wa Russia katika Shirika la NATO huko mjini Bruussels, amesema kuwa, uamuzi huo umechukkuliwa bila ya sababu za msingi wala ushahidi.  Aidha amesema:  Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa Shirika la Kijeshi la NATO amepokea maagizo ya kushadidisha mzozo na mvutano baina ya pande mbili na anakusudia kufikia lengo hilo katika kipindi cha muda mfupi.

lavrov

Sergei Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia

 

Katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano wa Russia na Shirika la NATO umechukua mkondo wa mzozo na mvutano hasa baada ya mgogoro wa Ukraine mwaka 2014. Kila mwaka kumekuwa kukishuuhudiwa kuongezeka kiwango cha migongano na makabiliano baina ya pande mbili, kiasi kwamba, kila upande umekuwa ukionya kuhusiana na kushadidi hali hii. Sababu ya kuongezeka mzozo huo, ni msimamo wa Russia wa kukosoa hatua ya madola ya Ulaya ya kuifuata kibubusa Marekani pamoja na siasa zake hususan kuhusiana na masuala ya kiusalama na kijeshi katika fremu ya NATO.

Kwa mtazamo wa viongozi wa Moscow ni kuwa, NATO imekuwa ikifanya mambo ambayo yanapelekea kuongezeka mizozo na hitilafu bila ya kuzingatia matakwa na maslahi ya Russia. Jambo jingine ambalo daima limekuwa likikosolewa na Russia, ni juhudi mtawalia za Shirika la Kijeshi la NATO za kusonga mbele kuelekea mashariki. Russia inaamini kwamba, hatua ya NATO ya kusonga mbele kuelekea mashariki ni tishio kwa usalama wake wa kitaifa na inaamini kwamba, utendaji wa NATO wa kupanua na kuongeza wanachama wa mkataba huo wa kijeshi ndio sababu ya kushadidi mizozo na mivutano.

 

Sergei Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia hivi karibuni alikosoa harakati za NATO jirani na mipaka ya Russia na Belarus na kusema kuwa,  kwa muda sasa nchi wanachama wa NATO zimeimarisha harakati zao za kijeshi katika mamlaka ya wanachama wapya wa umoja huo jirani na mipaka ya Russia na Belarus.

Ukweli wa mambo ni kuwa, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, madola ya Magharibi yakiwa na lengo la kuiondoa ulingoni Russia na kuidhoofisha kadiri inavyowezekana yameshadidisha mashinikizo ya kisiasa na kijeshi dhidi ya Moscow, kiasi kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, uhusiano wa pande mbili umekumbwa na hali mbaya kutokana na kuwekeana vikwazo, kufukuzwa wanadiplomasia, tuhuma za kuingilia uchaguzi, ujasusi na hujuma za kimtandao. Hata hivyo, inaonekana kuwa, kusimamishwa ushirikiano wa Russia na NATO, kumeufanya uhusiano wa pande mbili, uingie katika hatua mpya na hatari zaidi na hii inaashiria kushadidi zaidi hitilafu na mivutano baina ya pande mbili.

Tags