Oct 19, 2021 13:24 UTC
  • Korea Kaskazini yavurumisha baharini kombora jingine la balestiki

Kwa mara nyingine tena, jeshi la Korea Kaskazini limevurumisha baharini kombora jingine la balestiki katika pwani ya mashariki ya nchi hiyo.

Korea Kaskazini imevurumisha kombora hilo saa chache baada ya maafisa wa Marekani kudai kuwa Washington imejitolea kwa dhati kuhuisha mazungumzo ya nyuklia ya Pyongyang, yaliyogonga kisiki tangu wakati wa utawala wa Donald Trump.

Maafisa wa serikali za Korea Kusini na Japan wanasema jaribio hilo la kombora la balestiki limefanyika mwendo wa saa nne na robo asubuhi kwa saa za kanda hiyo, katika eneo la Sinpo, ambalo Korea Kaskazini hutumia mara kwa mara kuvurumisha makombora yake ya kutoka kwenye nyambizi.

Korea Kaskazini jana Jumatatu ilisema ipo tayari kurejea katika meza ya mazungumzo na Marekani pasi na masharti yoyote.

Kombora ya balestiki la Korea Kaskazini

Mwishoni mwa mwezi uliopita pia, Pyongyang ilitangaza kuwa imefanikiwa kurusha kombora jingine la balestiki aina ya hypersonic liitwalo Hwasong-8.

Korea Kaskazini imekuwa ikiendelea kustawisha uwezo wake wa silaha za makombora tangu yalipokwama mazungumzo ya kuishinikiza itokomeze silaha zake za nyuklia na makombora ya balestiki mkabala wa kupunguziwa vikwazo vilivyolemaza uchumi wa nchi hiyo.

Tags