Oct 20, 2021 07:20 UTC
  • Ugiriki, Misri na Cyprus zaionya Uturuki iache vitendo vyake vya kichokozi

Wakuu wa nchi za Cyprus, Misri na Ugiriki jana Jumanne walikutana mjini Athens na kutoa onyo kali kwa Uturuki iache vitendo vyake vya kichokozi katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterranean.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, katika tamko lao la Kikao cha Tisa cha Wakuu wa nchi hizo tatu, Ugiriki, Cyprus na Misri zimeitaka Uturuki iheshimu sheria za kimataifa na iache kukwamisha safari na kazi za meli za utafiti zinazofanya kazi zao katika bahari za Cyprus na Ugiriki.

Onyo hilo limesema pia kuwa, haiwezekani kuweko mazungumzo ya maana na ya utatuzi wa mambo iwapo Uturuki itaendelea kutoa vitisho na kukwamisha shughuli za meli za utafiti za nchi hizo.

Uturuki yatuhumiwa kwa kufanya uchimbaji katika eneo la kiuchumi la Cyprus

 

Jambo jengine lililotolewa onyo na wakuu wa nchi tatu za Misri, Ugiriki na Cyprus ni hatua ya meli za Uturuki kuchimba kinyume cha sheria katika eneo la kiuchumi la Ugiriki. Nchi hizo tatu zimelaani pia hatua ya Uturuki ya kuingia mara kwa mara kwenye anga ya Ugiriki bila ya idhini ya nchi hiyo na pia kufanya shughuli zilizo kinyume cha sheria kwa madhara ya Ugiriki na kinyume na sheria za kimataifa.

Wakati huo huo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya nao wamefikia uamuzi wa kuiwekea vikwazo Uturuki iwapo itaendelea na vitendo vyake vya uchochezi dhidi ya Cyprus.

Katika kikao chake kilichofanyika huko Luxembourg juzi Jumatatu, Umoja wa Ulaya ulimtaka Josep Borrel, Mkuu wa Sera za Kigeni wa umoja huo awasilishe mapendekezo yao kwa Umoja wa Ulaya kuhusu hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya Uturuki kwa uchochezi wake huo.

Tags