Oct 20, 2021 13:11 UTC
  • Waliofariki dunia kwa mafuriko na maporomoko ya ardhi India na Nepal wapindukia watu 100

Zaidi ya watu 100 wamefariki dunia baada ya siku kadhaa za mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi yaliyoharibu barabara na nyumba nchini India na Nepal.

Mamlaka za nchi hizo zimetangaza leo kuwa watu wengine wengi bado hawajulikani waliko.

Hadi kufikia leo, idadi rasmi ya waliofariki dunia nchini India imefikia 85 na 11 hawajulikani waliko na nchini Nepal idadi ya vifo imeongezeka hadi 31 na 43 hawajulikani waliko.

Mamlaka ya hali ya hewa nchini India imeongeza muda wa tahadhari yao Jumanne wiki hii na kutabiri kuwa mvua kubwa zitanyesha katika ukanda huo kwa siku mbili zijazo.

Katika eneo la Uttarakhand kaskazini mwa India, viongozi wamesema watu 46 walifariki dunia katika siku za hivi karibuni na 11 hawajulikani waliko. Katika jimbo la pwani la Kerala (Kusini), mkuu wa serikali katika jimbo hilo, Pinarayi Vijayan, ameitaja idadi ya vifo kuwa ni 39.

Mvua za mafuriko India

Karibu watu 30 walipoteza maisha huko Uttarakhand mapema jana katika matukio saba tofauti katika mkoa wa Nainital ulioathiriwa vibaya baada ya maporomoko ya ardhi na kuharibiwa kwa miundombinu, hali ambayo ilisababishwa na mafuriko makubwa.

Watu watano wa familia moja walifukiwa katika nyumba yao, amesema afisa wa eneo hilo, Pradeep Jain.

Waathiriwa wengine watano waliuawa katika maporomoko ya ardhi yaliyotokea wilayani Almora, kaskazini mwa Uttarakhand, na nyumba yao kuzama chini ya mawe na matope.

Kwa sababu ya indhari iliyotolewa kuhusiana na hali ya hewa, mamlaka zimeamuru shule zifungwe na kupiga marufuku shughuli zote za kidini au za watalii katika jimbo hilo.../

Tags