Oct 21, 2021 07:27 UTC
  • Taarifa ya kikao cha Moscow yataka kuundwa serikali shirikishi Afghanistan

Washiriki katika kikao cha Moscow wamesisitiza katika taarifa yao ya pamoja kuhusu udharura wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi ya Afghanistan na kutilia mkazo hamu yao ya kudumisha amani huko Afghanistan katika kanda hiyo nzima.

Kikao cha tatu cha mashauriano kuhusu Afghanistan kilifanyika jana mjini Moscow huko Russia kwa kikihudhuriwa na wajumbe maalumu au maafisa wa ngazi za juu wa nchi za Russia, China, Pakistan, Iran, India, Kazakhstan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan na pia ujumbe wa ngazi ya juu wa kundi la Taliban. 

Washiriki katika kikao cha Moscow kuhusu Afghanistan 

Washiriki katika kikao cha Moscow wamesisitiza katika taarifa yao ya pamoja kwamba wanaheshimu mamlaka ya kujitawala, uhuru na umoja wa ardhi nzima ya Afghanistan. Aidha wamesisitiza azma yao ya kuhakikisha kuwa Afghanistan inakuwa nchi ya amani, isiyokubali kugawanywa, yenye maendeleo ya kiuchumi, huru na pasina ugaidi na uhalifu unaohusiana na madawa ya kulevya na yenye kuheshimu misingi mikuu ya haki za binadamu.  

Nchi washiriki katika kikao cha Moscow kuhusu Afghanistan pia zimewatolea wito viongozi wa Kiafghani kuchukua hatua zadi ili kuimarisha mamlaka na kuunda serikali shirikishi yenye kuakisi maslahi ya makundi yote ya kisiasa na kikaumu ya nchi hiyo.

Katika upande mwingine nchi hizo zimesema kuwa zina wasiwasi na hali mbaya ya kiuchumi na kibinadamu huko Afghanistan na kueleza kuwa, kuna udharura kwa jamii ya kimataifa kufanya juhudi za kufanikisha misaada ya kibinadamu na kiuchumi kwa wananchi wa Afghanistan wakati huu wa kuijenga upya nchi hiyo baada ya mapigano ya miaka kadhaa. 

Taarifa ya pamoja ya kikao cha Moscow imesema: Jukumu kuu la masuala ya kiuchumi na kuijenga upya Afghanistan baada ya vita linapaswa kuchukuliwa majeshi yaliyoivamia nchi hiyo kwa kipindi cha miaka ishirini.