Oct 21, 2021 11:51 UTC
  • Korea Kaskazini yaitaka Marekani iache undumakuwili kuhusu makombora

Korea Kaskazini imeituhumu Marekani kuwa inatumia sera za undumakuwili kuhusu mpaango wa silaha za Pyongyang.

Katika taarifa Ahamisi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini, ambaye jina lake halikutajwa, amenukuliwa na Shirika la Habari la Korea (KCNA) akisema Marekani imekuza mambo kwa kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya Pyongyang kufanya jaribio  la kombora hivi karibuni.

Siku mbili zilizopita Korea Kaskazini ilifanyia majaribio kombora jipya la kurushwa kutoka katika nyambizi (SLBM).

Msemaji huyo amesema jaribio hilo limefanyika kwa msingi wa kuihami nchi na halikuwa limeelekezwa kwa Marekani au nchi nyingine.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un akiwa katika eneo la jaribio la kombora baharini

Amesema kombora ambalo Korea Kaskazini imelifanyia jaribio ni sawa na makombora yanayomilikiwa na Marekani hivyo kubainisha wasiwasi kuhusu jairibio hilo ni undumakuwili.

Afisa hiyo wa Korea Kaskazini amesema hatua ya Marekani kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni uchochezi ambao unaweza kuwa na madhara makubwa.

Katika wiki za hivi karibuni Korea Kaskazini imefanyia majaribio makombora ya msafa marefu ya cruise likiwemo kombora ambalo linaweza kurushwa kutoka katika gari moshi na jingine ambalo lina kasi mara tano zaidi ya sauti.