Oct 22, 2021 07:10 UTC
  • Rais Putin wa Russia apongeza nafasi ya Hizbullah katika siasa za Lebanon

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ina nafasi muhimu katika uga wa kisiasa nchini Lebanon.

Ameyasema hayo Alhamisi katika kikao cha Klabu ya Mazungumzo ya Valdai katika mji wa Sochi nchini Russia na kuongea kuwa: "Nafahamu vyema kuwa watu tafauti katika nchi tofauti wana mitizamo tofauti kuhusu Hizbullah."

Putin amesema kwa matazamo wa Russia, Hizbullah ni nguvu muhimu ya kisiasa nchini Lebanon na kuongeza kuwa, Russia inawasiliana na makundi yote yenye nguvu za kisiasa Lebanon na itaendelea kufanya hivyo.

Aidha amesema Russia inataka kuona pande zote za kisiasa Lebanon zinafikia mapatano bila mapigano na kuongeza kuwa, Moscow inashirikiana na Walebanon wote kuzuia umwagikaji damu nchini humo.

Mlipuko katika Bandari ya Beirut

Kauli ya Putin imekuja baada ya watu saba kuuawa shahidi na wengine 60 kujeruhiwa Oktoba 14 wakati wafuasi wa Hizbullah walipokuwa wakiandamana kwa amani dhidi ya jaji anayechunguza mlipuko katika Bandari ya Beirut mwaka jana ambaye anatuhumiwa kupendelea upande mmoja. Waliouawa katika hujuma hiyo aghalabu walikuwa ni wafuasi wa Harakati ya Hizbullah.

Putin amesema hawezi kutoa tamko kuhusu masuala ya kisiasa yanayofungamanishwa na idara ya mahakama ya Lebanon lakini ameongeza kuwa, mlipuko wa Bandari ya Beirut unahusishwa na baadhi waliotaka kupata faida kwa kuuza fataliza kwa bei ya juu.