Oct 22, 2021 13:06 UTC
  • Kikao cha Moscow kuhusu Afghanistan na juhudi za kurejesha uthabiti nchini humo

Kikao cha Moscow kuhusu Afghanistan kilifanyika siku ya Jumatano ya tarehe 20 Oktoba kwa uwenyekiti wa Russia katika mji mkuu huo wa nchi hiyo.

Hicho kilikuwa kikao cha tatu cha mashauriano ya "mduara wa Moscow" kuhusu Afghanistan, kilichofanyika kwa kuhudhuriwa na wawakilishi maalumu na maafisa waandamizi wa Russia, China, Iran, Pakistan, India, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan pamoja na ujumbe wa ngazi ya juu wa serikali ya muda ya Afghanistan.

Katika taarifa yao ya pamoja, washiriki wa kikao cha Moscow walitilia mkazo kuheshimiwa mamlaka na uhuru wa kujitawala wa Afghanistan na kusisitizia pia azma yao ya kusaidia kurejesha amani katika maeneo yote ya nchi hiyo, kuundwa serikali shirikishi na vile vile kuchangia kupatikana uthabiti katika eneo. Marekani ilikataa kuhudhuria kikao hicho cha Moscow.

Kikao cha Moscow kuhusu Afghanistan

Inavyoonyesha, kikao cha Moscow kuhusu Afghanistan ni mwendelezo wa juhudi za Russia za kurejesha uthabiti ndani ya Afghanistan, kuzuia kusambaa wimbi la hali ya mchafukoge, kuimarisha usalama na vilevile kuharakisha mchakato wa kuundwa serikali pana na jumuishi nchini humo. Hii ikiwa na maana ya kufanya jitihada za kushirikiana na Taliban na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kurekebisha na kuweka sawa hali ya mambo katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita. Kwa sababu hiyo, jitihada za Russia zimejikita katika kufanya mazungumzo na Taliban na kulishinikiza kundi hilo liendeshe utawala kwa sura yenye muelekeo, kwa namna fulani, wa kidemokrasia ili kuhakikisha hali ya mchafukoge na wimbi jipya la wakimbizi haviibuki tena nchini Afghanistan. Zamir Kabulov, mwakilishi wa rais wa Russia katika masuala ya Afghanistan amethibitisha kuwa kundi la Taliban lilialikwa rasmi kuhudhuria kikao cha Moscow.

Tangu Taliban iliposhika hatamu za madaraka nchini Afghanistan mwezi Agosti mwaka hu, Russia imekuwa na msimamo wenye mielekeo miwili kuhusiana na kundi hilo. Moscow imekubali kuwa Taliban ni uhalisia uliopo Afghanistan na imekuwa tayari kufanya kazi na kundi hilo. Lakini hiyo haimaanishi kulitambua kundi hilo kama serikali halali na inayotokana na wananchi. Msimamo huo umesisitizwa mara kadhaa na maafisa waandamizi wa kisiasa wa Russia. Kazi ya msingi inayofanywa na Moscow, ni kuwa na mawasiliano ya karibu na Taliban. Katika kikao hicho cha Moscow, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov aliashiria jitihada zinazofanywa na serikali ya muda ya Afghanistan za kurejesha uthabiti wa kisiasa na kiusalama nchini humo na kusisitiza kwa kusema: "Matarajio yetu ni kuona harakati ya Taliban inaunda serikali jumuishi itakayoshirikisha makundi yote ya kisiasa ndani ya Afghanistan. Pamoja na hayo, kurejesha amani na usalama nchini Afghanistan, lingali ni jukumu kuu na la msingi zaidi la viongozi wapya wa Kabul." 

Sergey Lavrov

Sambamba na hayo tukumbuke pia kwamba, kwa muda mrefu wakati wa urais wa Donald Trump, Marekani ilikuwa ikiituhumu Russia kuwa ina mawasiliano na Taliban na hata kulipatia fedha kundi hilo liwaue askari wa Marekani. Kwa muktadha huo, uhusiano mzuri unaoshuhudiwa baina ya Moscow na Taliban katika zama hizi mpya haliwezi kuwa jambo la ajabu. Na kama ilivyotarajiwa, uhusiano wa pande hizo mbili ni wa maelewano mazuri; na inachopigania Russia kwa kushirikiana na China ni kutaka kujaza nafasi tupu iliyoachwa na Marekani na waitifaki wake wa Magharibi nchini Afghanistan.

Suala jengine muhimu kwa Russia kuhusu Afghanistan ni wasiwasi ilionao juu ya kushamiri vitendo vya kigaidi vya kundi la ukufurishaji la DAESH (ISIS) na kusambaa hadi nchi jirani katika eneo la Asia ya Kati, yaani Tajikistan na Uzbekistan na kutokea huko hadi nchi zingine ikiwemo Russia. Pir Muhammad Mulla Zahi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Warusi wana wasiwasi makundi yaliyojiimarisha kama DAESH kuitumia hali ya mchafukoge iliyopo ndani ya Afghanistan na kuweza kuingia eneo la satua ya Russia kupitia kaskazini, yaani Asia ya Kati na Caucasia. Kwa hivyo wanataka kuhakikisha Taliban inaweza kuzatiti nguvu na mamlaka yake katika ardhi yote ya Afghanistan."

 

Ujumbe wa Taliban katika kikao cha Moscow

Russia imedhamiria kuhakikisha inachukua hatua yoyote inayohitajika kwa njia ya moja kwa moja au kupitia jumuiya ya makubaliano ya usalama wa pamoja ili kulinda usalama wa nchi za muungano wa zamani wa Shirikisho la Kisovieti katika Asia ya Kati dhidi ya vitisho vya Daesh. Kufanyika kikao cha Moscow kuhusu Afghanistan ni uchukuaji hatua moja mbele kwa ajili ya kufikia mwafaka wa pamoja na kuratibu ramani ya njia ili kwa mashauriano ya pamoja ya nchi jirani na zinazopakana na Afghanistan kuhakikisha uthabiti unarejea katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita sambamba na kurejeshwa amani na kuundwa serikali shirikishi nchini humo.../

Tags