Oct 23, 2021 00:21 UTC
  • Kremlin yasisitiza kusitisha mazungumzo na muungano wa NATO

Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin) amesema kuwa mpango mpya wa kiulinzi wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) unaopnyesha kuwa, uamuzi uliochukuliwa na Moscow wa kusimamisha mazungumzo na jumuiya hiyo ulikuwa sahihi kikamilifu.

Dmitry Peskov alisema jana Ijumaa katika kikao na waandishi wa habari kwamba, mpango mpya wa kiulinzi wa muungano wa Nato unasadikisha uamuzi sahihi uliochukuliwa na Russia siku kadhaa zilizopita kuhusu kuhitimisha mazungumzo rasmi na NATO. Amesema, katika mazingira kama haya hakuna haja ya kufanya mazungumzo. 

Msemaji wa Kremlin ameongeza kuwa, Moscow inaamini kuwa muungano huo wa kijeshi wa nchi za Magharibi uliasisiwa kwa ajili ya kupambana na pande nyingine.

Wiki iliyopita Russia ilisimamisha shughuli za Ofisi ya Intelijinsia ya NATO mjini Moscow na uwakilishi wa kudumu wa Russia katika muungano huo ikiwa ni jibu lake kwa hatua ya NATO ya kufuta hati za utambulisho za wafanyakazi wa ofisi ya mwakilishi wa Russia katika muungano huo. 

Mwakilishi wa Russia katika muungano wa NATO, Alexander Grushko amesema kuhusu suala hilo kwamba, uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia kati ya Moscow na NATO hauwezekani tena kutokana na vitendo visivyo vya kirafiki vilivyodhihirishwa na jumuiya hiyo hivi karibuni mkabala wa Russia. 

Mwakilishi wa Russia katika muungano wa Nato, Alexander Grushko

Juzi Alhamisi afisa mmoja wa ngazi ya juu wa NATO alisema kuwa, muungano huo unatekeleza mkakati wa kuanzisha nguvu ya kukabiliana na Russia.