Oct 23, 2021 07:48 UTC
  • DAESH lakiri kuhusika na hujuma ya kuripua kinu cha umeme mjini Kabul, Afghanistan

Kundi la kigaidi na ukufurishaji la DAESH (ISIS) limekiri kuwa ndilo lililohusika na shambulio la kinu kikuu kinachozalisha umeme katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, kundi hilo la kigaidi limeeleza katika taarifa kwamba, siku ya Alkhamisi, wanachama wake walitega na kuuripua bomu kwenye jengo la usambazaji umeme katika mji wa Kabul.

Shirika la umeme la Afghanistan lilitangaza hapo kabla kuwa, mripuko uliotokea katika kinu cha umeme umesababisha kukatika nyaya za kusambaza umeme katika mji mkuu Kabul na mikoa mingine jirani.

Hujuma hiyo ya kigaidi ya kundi la ukufurishaji la Daesh imefanywa katika hali ambayo kiwango kikubwa cha umeme unaotumika nchini Afghanistan kinaagizwa kutoka nchi jirani za Uzbekistan, Tajikistan na Iran; na mara kwa mara nyaya za usambazaji umeme nchini humo huwa zinaharibiwa kwa hujuma na mashambulio.

Mnamo mwezi Februari mwaka huu pia mitambo minne ya umeme iliharibiwa na umeme unaosambazwa kutoka Kabul kuelekea mkoa wa Ghazni ulikatika baada ya kutokea mapigano kati ya wapiganaji wa kundi la Taliban na wa vikosi vya serikali ya wakati huo ya Afghanistan.../

Tags