Oct 23, 2021 15:43 UTC
  • Rais wa China, Xi Jinping
    Rais wa China, Xi Jinping

Serikali ya China imejibu matamshi yaliyotolewsa majuzi na Rais Joe Biden wa Marekani kuhusu Taiwan na kumtaka awe na tahadhari zaidi. Beijing imesisitiza kuwa, haitalegeza kamba wala kufanya suluhu kuhusiana na masuala ya kimsingi kama mamlaka yake na mipaka ya ardhi ya nchi hiyo.

Hivi karibuni Rais Joe Biden alisema kuwa, iwapo jeshi la China litaishambulia Taiwan basi Marekan itakuwa tayari kukilinda kisiwa hicho. Wakati huo huo mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa ameitahadharisha serikali ya Washington isije ikakitumbukiza kisiwa hicho katika vita. China inaitambua Taiwan kuwa ni sehemu ya ardhi ya nchi hiyo na inafanya mikakati ya kukiunganisha tena na ardhi mama kupitia sera za China Moja na Mifumo Miwili kama ilivyofanya kuhusiana na Hong Kong na Macao. Hata hivyo Marekani ambayo miaka ya karibuni imepatwa na wasiwasi mkubwa kuhusiana na kuporomoka ushawishi wake duniani kutokana na kasi ya ustawi na maendeleo ya China, imezidisha sana mashinikizo dhidi ya Beijing kupitia njia ya kustawisha zaidi ushirikiano wake na Taiwan na kuzidisha uwezo wake sa kijeshi mkabala wa China. Hata hivyo Washington haiwezi kupuuza umuhimu wa kuwepo ushirikiano na Beijing katika masuala mbalimbali ya kimataifa. 

Fredric Camp ambaye ni mtaalamu wa siasa za Marekani anasema: "Uhusiano wa Marekani na China unaathiri masuala mengi ya kimataifa kwa kipindi cha sasa na hata katika siku za usoni. Kwa msingi huo una umuhimu mkubwa na wa aina yake." 

Japokuwa Joe Biden ameitahadharisha China isiishambuli Taiwan lakini ni wazi kuwa, Washington imeonesha kivitendo kwamba, haina hamu ya kuingia vitani katika makabiliano ya kijeshi na nchi hiyo. Hadi sasa jamii ya kimataifa bado haijasahau jinsi China ilivyoidhalilisha Marekani baada ya kuchukua ndege ya kijeshi ya nchi hiyo iliyoingia katika ardhi ya China na kuisambaratisha vipande vipande kisha ikavikabidhi kwa jeshi Marekani. Hii ina maana kwamba, Marekani inaelewa vyema jinsi China inavyolipa umuhimu mkubwa suala la kisiwa cha Taiwan, na vilevile inaelewa vyema kwamba, vyovyote vile utakavyokuwa umuhimu wa Taiwan kwa Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla, lakini haina thamani na kulitumbukiza jeshi la nchi hiyo katika vita vya pande zote na nchi ya China ambavyo hapana shaka kuwa vitaziburuta pia nchi kama Japan na Korea Kusini katika uwanja wa mapigano.

Alaa kulli hal, China imeonesha kivitendo kwamba, japokuwa imekubali kulegeza kamba mkabala wa Marekani katika masuala kama ya ushindani wa kiuchumi lakini haiko tayari hata kidogo kusalimu amri au kulegeza kamba mbele ya mashinikizo ya aina yotote katika masuala yanayohusiana na mamlaka na ardhi ya nchi hiyo ikiwemo kadhia ya Taiwan. Kwa sababu hiyo pia serikali inayotaka kujitenga ya kisiwa cha Taiwan imekuwa na tahadhari kuhusu suala la kujitangazia uhuru na kujitenga na China. Na kwa msingi huo imejiepusha kuathiriwa na siasa na sera zisizo imara za serikali ya Marekani za eti kukilinda kisiwa hicho.   

Tags