Oct 24, 2021 02:25 UTC
  • Madai ya Ufaransa kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran, kuendelezwa sera za kindumakuwili za Ulaya

Sambamba na mkutano wa Ijumaa ya wiki hii baina ya wawakilishi wa Marekani na nchi za Ulaya uliofanyika mjini Paris, Ufaransa imeitaka Iran ipunguze shughuli zake za kuzalisha nishati ya nyuklia.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Ufaransa, Anne-Claire Legendre amedai kuwa Iran imekiuka makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuitaka Tehran ishirikiane kikamilifu na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Ufaransa amekwepa kuashiria jinsi nchi za Magharibi zilivyokiuka makubaliano hayo na kuacha kutekeleza majukumu yao. Legendre pia amedai kuwa, Marekani na Ulaya ziko tayari kurejea mara moja kwenye meza ya mazungumzo na Iran ili kufikia mapatano ya kuifanya Tehran itekeleze majukumu yake na kuirejesha Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. 

Hapana shaka kuwa kurejea kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuna umuhimu mkubwa kwa sharti kwamba, mazungumzo hayo yawe na matokeo ya kivitendo katika kudhamini maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hata hivyo hadi sasa Marekani na nchi tatu za Ulaya wanachama katika makubaliano hayo hazijachukua hatua ya maana katika uwanja huo. 

Paris inayojidhihirisha kuwa ina wasiwasi kuhusu suala la kucheleweshwa mazungumzo hayo, imeonesha misimamo inayokinzana katika kadhia hiyo. Inaonekana kuwa maafisa wa serikali ya Paris wamesahau au wanajisahaulisha kwamba, Marekani ndiyo iliyoanza kukiuka makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Baada ya hapo pia troika ya Ulaya haikuchukua hatua yoyote ya kutekeleza majukumu yake katika mkataba huo hususan katika upande wa kudhamini maslahi ya Iran. Hivyo inaonekana kuwa, nchi hizo za Ulaya zinatoa taarifa za mara kwa mara ili kupotosha fikra za walimwengu na kuhalalisha ukiukaji wao wa mkataba huo. Mienendo hiyo inaonesha kuwa, Marekani na nchi za Ulaya zinataka kuanzisha hali mpya chini ya mwavuli wa mazungumzo ya kuhuisha mapatano ya JCPOA. 

Tarehe 8 Mei mwaka 2018 Marekani ilijiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa licha ya Wakala wa kKimataifa wa Nishati ya Nyuklia kuthibitisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu imetekeleza majukumu yake yote katika mkataba huo.

Hadi sasa kumefanyika duru sita za mazungumzo ya kujaribu kuhuisha makubaliano hayo na kuirejesha Marekani kwenye JCPOA katika mji wa Vienna huko Austria, lakini hadi sasa hayajazaa matunda ya kuridhisha. Sasa Marekani na Ulaya zinaitaka Iran eti irejee kwenye meza ya mazungumzo huko Vienna na sambamba na hayo zinaiwekea Tehran vikwazo vipya, suala ambalo ni kielelezo cha mgongano uliopo katika mienendo ya nchi hizo. Mienendo hiyo pia haitoi ujumbe mzuri kwa serikali ya Iran.

Vienna

Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaliyopasishwa na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yameainisha majukumu ya kila upande; hata hivyo Ulaya na Marekani zimeyaefanya rehani wa maslahi yao. Kuendeleza sera za huko nyuma na kuendelea kutoa tuhuma zisizo na msingi kuhusu shughuli za kuzalisha nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani za Iran kutatoa pigo zaidi kwa makubaliano hayo.

Akizungumzia misimamo ya kukinzana ya nchi za Ulaya kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na swali kwamba kwa nini nchi hizo, kwa upande mmoja zinasisitiza udharura wa kulindwa makubaliano hayo na kwa upande mwingine zinafuata sera za vikwazo za Marekani, mchambuzi wa Kifaransa, Alexandre Austin amesema kuwa, tangu kulipofutwa vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran nchi za Ulaya zilijiunga na Marekani katika sera zake za vikwazo dhidi ya Iran na kwamba misimamo hiyo ya kindumakuwili na ya kukinzana si sahihi na haikubaliki.

Wakati Marekani ilipojiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuanzisha tena vikwazo dhidi ya Iran, nchi za Ulaya ziliamua kujiondoa katika soko la Ulaya kwa kuhofia kupoteza soko la Marekani. Kwa maneno mengine ni kuwa, nchi hizo za Ulaya pia zilikuwa mhanga wa sera za vikwao za Marekani.

Alexandre Austin anasema kuwa: "Ulaya inaweza kupambana na mashinikizo ya Marekani iwapo itashikama na kuwa na umoja, lakini tatizo lililopo ni kwamba nchi hizo za Ulaya zinasumbuliwa na migawanyiko na ukosefu wa umoja."

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran Hossein Amir Abdollahian alisema hivi karibuni akiwa safarini mjini Moscow kwamba: "Kama mazungumzo ya Vienna yamepangwa kufanyika kwa kipindi cha miaka nane, na mazungumzo yafanyike tu kwa ajili ya mazungumzo, basi Jamhuri ya Kiislamu itachukua uamuzi mwafaka kwa wakati wake."

Hossein Amir Abdollahian

Msimamo huo unaonesha kuwa, stratijia ya Tehran kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA iko wazi na ni ya kimantiki na kwamba kurejea Iran katika meza ya mazungumzo hayo kutategemea azma na nia njema ya upande wa pili.         

Tags