Oct 24, 2021 03:26 UTC
  • Iran yaadhimisha siku ya kuzaliwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw)

Leo tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiu Awwal 1443 Hijria inasadifiana na siku aliyozaliwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad bin Abdullah (saw) na mjukuu wake mwema, Imam Ja'far al Swadiq (as).

Maulama na wanahistoria wengi wa Kiislamu wanasema kuwa, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Mwaka wa Tembo katika mji mtakatifu wa Makka. Baadhi ya wasomi hao wamesema alizaliwa tarehe 12 mwezi huo huo, na kwa msingi huo mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Ruhullah Khomeini aliitangaza wiki moja ya kuanzia tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal kuwa Wiki ya Umoja baina ya Waislamu na siku za kusherehekea na kuadhimisha kuzaliwa kwa mtukufu huyo.

Katika kipindi cha mwanzoni mwa ujana wake, Muhammad Mwaminifu alikuwa akijitenga na jamii ya kijahilia ya watu wa Makka na kwenda kwenye pango la Hiraa lililoko karibu na mji huo na kuketi huko kwa masaa kadhaa akitafakari katika maumbile ya dunia na kufanya ibada. Mtukufu huyo alipewa utume akiwa na umri wa miaka 40. 

Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) alikumbana na mashaka mengi katika jitihada zake za kufuta ibada ya masanamu, ujinga, umaskini na kadhalika na alifanya jitihada kubwa za kueneza imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja, kupambana na dhulma na unyanyasaji na kueneza uadilifu, umoja, amani na mshikamano baina ya wanadamu. 

Muhammad (saw) alikuja na kitabu kitakatifu cha Qur'ani kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambacho ndicho kitabu cha mwisho na kamili zaidi cha Mwenyezi Mungu. Mafundisho ya mtukufu huyo yalihimiza kuheshimiwa kiumbe mwanadamu, kuwakirimu wanawake na wasichana ambao walikuwa wakizikwa wakiwa hai katika jamii ya Bara Arabu na kueneza maadili mema. 

Mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (saw) Imam Ja'far Swadiq (as) pia alizaliwa siku kama hii ya leo tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina.

Kwa minasaba ya siku hii ya sherehe za Maulidi na kuzaliwa Mbora wa Viumbe Muhammad Mwaminifu (saw) na mjukuu wake, Imam Swadiq (as), Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani.

Tags